Na Timothy Itembe Tarime.
UMOJA wa kikundi cha Waandishi wa Habari na Wapiga Picha (REU) Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, kimelaani maandamano yanayodaiwa kutokuwa na baraka za Serikali, huku kikitoa wito kwa taasisi zote kuheshimu kazi za waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza kwa niaba ya kikundi hicho, Mwenyekiti wa REU Tarime, Jacob Kalori, alisema waandishi wa habari wanatambuliwa kikatiba kupitia Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, zinazowapa haki ya kukusanya, kuchakata na kusambaza habari kwa kuzingatia sheria za nchi.
Kalori alisema msimamo huo umetolewa kufuatia kauli aliyoitoa jana wakati wa mazishi ya dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, marehemu Swezi Dandel Maradufu.
Alisema kumekuwa na matukio ya waandishi wa habari kuingia katika misuguano na askari polisi wanapotekeleza majukumu yao ya kikazi, hali ambayo, kwa mujibu wake, ni kinyume na haki za msingi zinazolindwa na Katiba ya nchi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata na kusambaza taarifa.
"Waandishi wa habari wanapaswa kupewa nafasi ya kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria bila vikwazo visivyo vya lazima.Tunatoa wito kwa taasisi zote za Serikali na binafsi kuheshimu haki na wajibu wa waandishi wa habari kama inavyotambuliwa na Katiba na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016,"alisema Kalori.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Mark Njera, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, kwa juhudi wanazozifanya katika kusimamia ulinzi na usalama ndani ya wilaya hiyo.
Wakati huo huo, wazee wa mila wa koo 13 za kabila la Wakurya wilayani Tarime wametoa wito kwa wananchi kutumia Julai 7, 2026, kama siku ya mapumziko na amani, badala ya kushiriki katika shughuli zozote zinazoweza kuvuruga utulivu.
Akizungumza kwa niaba ya wazee hao katika mkutano uliohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi,Mzee Mwita Nyanteto wa Nyamongo alisema tarehe hiyo imewekwa kwa mujibu wa mila kuwa siku ya mapumziko na ibada za kimila.
Alisema kwa mujibu wa utamaduni wao, siku hiyo hairuhusiwi kufanya kazi nzito, kubeba mizigo kichwani, kuchinja mnyama wala kufanya kitendo chochote kinachoashiria umwagaji wa damu, akisisitiza kuwa wa
