Ajira Milioni 230 za Kidijitali Zinakuja, Kikwete Aonya Afrika Kujiandaa


Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi ya Global Partnership for Education (GPE), taasisi ya kimataifa inayojihusisha na kuendeleza elimu duniani, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji katika elimu na maendeleo ya rasilimali watu ili kuandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa kidijitali.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kushiriki Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Dkt. Kikwete amesema dunia inatarajiwa kuwa na takribani ajira milioni 230 zinazohitaji ujuzi wa teknolojia za kidijitali ifikapo mwaka 2050.

Amesema hali hiyo inapaswa kuwa chachu kwa nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika kuwajengea vijana maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye, ili waweze kushindana na kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.

Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio ya Afrika katika karne ya 21 yatategemea uwezo wa kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, afya, uhandisi, usafirishaji na teknolojia.

Dkt. Kikwete ameeleza kuwa uwekezaji katika elimu unapaswa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani, akibainisha kuwa Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele katika kuandaa nguvu kazi yenye ushindani wa kimataifa.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi