Nchini Afrika Kusini, tishio la ghasia za kisiasa linaonekana kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 4, 2026. Kifo cha Aubrey Tsengwa, meya wa zamani wa ANC wa Knysna kusini mwa nchi, aliyepigwa risasi siku ya Jumatano jioni, Agosti 19, 2026, kimeibua wasiwasi. Chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana, na hakuna mtu aliyekamatwa.
Kulingana na matokeo ya awali ya uchunguzi, Aubrey Tsengwa alikuwa akiendesha gari lake akielekea nyumbani siku ya Jumatano jioni, akiandamana na watu wengine watatu, wakati mshambuliaji alipofyatua risasi kabla ya kukimbia kwa miguu. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 48 alipata "majeraha mengi ya risasi kichwani na sehemu ya juu ya mwili" na alitangazwa "amefariki katika eneo la tukio," kulingana na polisi.
Aubrey Tsengwa alikuwa meya wa jiji hili la pwani mashariki mwa Cape Town kuanzia mwaka 2022 hadi 2025, chini ya bendera ya ANC, kabla ya kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye. Wapinzani wake, ambao baadhi yao walikuwa wanachama wa muungano wake, walimtuhumu kwa utawala mbaya na uteuzi haramu wa wanachama wa timu yake. Tangu wakati huo alikuwa amerudi katika nafasi yake kama diwani wa kawaida wa jiji huko Knysna.
Ingawa sababu ya uhalifu huo haijulikani kwa sasa, mauaji hayo yanatokea kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa, uliopangwa kufanyika tarehe 4 Novemba 2026, katika muktadha wa mapambano ya kugombea madaraka na udhibiti wa zabuni za umma, hali inayozua hofu ya kuongezeka kwa ghasia za kisiasa."
Mwezi Juni mwaka huu, wawakilishi watatu wa vyama tofauti walipigwa risasi na kuuawa mwishoni mwa juma moja katika matukio matatu tofauti huko Cape Town na Port Elizabeth.
