Kuna taarifa inayosambaa kupitia mitandao ya kijamii iliyotolewa Oktoba 26, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Brenda Rupia ikijilisha umma kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu ameanza mgomo wa kula chakula kuanzia Oktoba 26, 2026 pamoja na kuzuiwa kwa mawakili wake wa tatu (3) kuingia gerezani. Kimsingi taarifa hizi si za kweli na zinatakiwa zipuuzwe kwani ni za upotoshaji na zenye kuleta taharuki katika jamii.
Jeshi la Magereza linapenda kuujulisha umma kwamba, Mahabusu Tundu Lissu yupo salama na hayupo katika mgomo wa kula chakula kama ilivyoripotiwa. Kuhusu kutembelewa na mawakili wanaomwakilisha wameendelea kuruhusiwa kuonana na mteja wao kwa mujibu wa taratibu baada ya kujiridhisha kuwa ni mawakili wake na si vinginevyo. Jambo hili limekuwa likitekelezwa kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo.
Vilevile, katika kutekeleza majukumu yake ya kuwapokea, kuwahifadhi na kuwarekebisha wale wote wanaoshikiliwa magerezani, wakati wote Jeshi limekuwa likizingatia mambo yote yanayohusu usalama wao kwa kipindi chote wanachokua chini ya ulinzi halali wa Jeshi la Magereza.
Hivyo, Jeshi linatoa rai kwa wananchi kupuuzia taarifa hiyo na kuacha kusambaza taarifa isiyo na ukweli kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Aidha, Jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ikiwemo suala la usalama na kuthamini utu na misingi ya haki za binadamu.
