Serikali yataja soko la mitaji chanzo muhimu cha fedha za maendeleo


Serikali imehimiza wananchi wengi zaidi kushiriki katika soko la mitaji kwa kuweka akiba na kuwekeza kwa muda mrefu, hatua inayolenga kuimarisha uchumi wao na kuongeza ukwasi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuorodheshwa kwa mfuko wa Zan Securities katika DSE, Kamishna wa Fedha za Nje na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Rished Bade, amesema hatua hiyo inachangia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha unaolenga kupanua ushiriki wa wananchi katika huduma rasmi za kifedha na kukuza soko la mitaji nchini.


Kwa upande wake, mwakilishi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaud Julius, ameipongeza Zan Securities kwa ubunifu huo, akieleza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuweka mikakati ya kuongeza bidhaa mpya katika soko la mitaji na dhamana nchini.

Aidha, Zan Securities Limited imesisitizwa kuhakikisha fedha za wawekezaji zinasimamiwa kwa uwazi, uadilifu na weledi, huku maslahi yao yakipewa kipaumbele na kuzingatiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Zan Securities, Bw. Raphael Masumbuko, amesema mfuko huo umeanzishwa kurahisisha uwekezaji kwa wananchi, hususan wawekezaji wadogo ambao hawana muda, utaalamu na nyenzo za kutosha kufanya utafiti na kufuatilia mifuko mbalimbali ya uwekezaji.

Amesema Zan Timiza ETF inawawezesha wawekezaji kununua kipande kimoja cha mfuko na kupata fursa ya kuwekeza katika mifuko mbalimbali ya uwekezaji kupitia utaratibu mmoja.







Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi