JIJI LA TANGA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA, WADAU WATAKIWA KUSHIRIKI

 


Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushiriki wa jamii nzima ili kukomesha vitendo hivyo haramu vinavyodhoofisha nguvu kazi na kuathiri maendeleo ya Halmashauri ya Jiji la Tanga.


Hayo yamesemwa na Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Khalid Rashid, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwanzange, wakati akifunga semina ya mafunzo ya siku tano iliyowashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo jijini humo.


Rashid alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, chini ya uongozi wa Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapher Selebos, hakuna kitakachoshindikana iwapo wadau watashirikiana kwa dhati.


Semina hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Red Cross jijini Tanga, chini ya uratibu wa asasi ya Gift of Hope, iliwashirikisha walimu, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa vijana, wakuu wa taasisi pamoja na waandishi wa habari.


Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwajengea uwezo washiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kuhakikisha Jiji la Tanga linakuwa eneo salama kwa wananchi.


Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Meya Rashid alisisitiza umuhimu wa kila mmoja kushiriki katika mapambano hayo, akisema ushirikiano huo utasaidia kukomesha vitendo vya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.


Alisema hali bado si nzuri katika Halmashauri ya Jiji la Tanga licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika, hivyo akasisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na wadau wote unahitajika zaidi.


"Naamini mafunzo haya ya siku tano mmeyapata kikamilifu. Msiyafungie kwenye makabati, bali mkayafanyie kazi kwa kuielimisha jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya," alisema Naibu Meya huyo.


Aidha, alisema jiografia ya Jiji la Tanga, ikiwemo ukaribu wake na nchi jirani ya Kenya pamoja na uwepo wa bandari, ni miongoni mwa sababu zinazoweza kutumiwa na wahalifu kama mianya ya kuingiza dawa za kulevya.


Hata hivyo, aliwataka wanaojihusisha na biashara hiyo haramu kuachana nayo mara moja, akieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.


Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la Jeshi la Polisi pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima, wakiwemo wananchi, viongozi wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali.


Pia aliipongeza asasi ya Gift of Hope kwa jitihada inazoendelea kuzifanya katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuiunga mkono ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.


Akifafanua umuhimu wa ushirikiano huo, Rashid alisema uwekezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati jijini Tanga unahitaji uwepo wa nguvu kazi yenye afya na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.


Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiletea nchi miradi mingi ya kimkakati inayohitaji vijana wenye afya njema na wasiokuwa katika matumizi ya dawa za kulevya ili waweze kunufaika na fursa za ajira zinazotokana na miradi hiyo.


Alionya kuwa vijana wasipojikinga na matumizi ya dawa za kulevya, wanaweza kupoteza fursa hizo na kuziacha zitumiwe na watu kutoka nje ya nchi.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Duga, Japhari Mohamed, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Uchumi na Afya, aliipongeza asasi ya Gift of Hope kwa jitihada zake za kupambana na dawa za kulevya.


Alisema amefurahishwa na mafunzo hayo na anaamini maarifa aliyoyapata yatasaidia katika kuelimisha jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.


Naye Mwalimu Yahaya Bakari alisema mafunzo hayo yamemuongezea maarifa yatakayomsaidia kusimamia nidhamu ya wanafunzi na kutambua viashiria vya awali vya tabia zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kujihusisha na dawa za kulevya.


Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii, Farida Adamjee, alisema semina hiyo imemwezesha kujifunza changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, akiahidi kutumia maarifa aliyoyapata katika kujenga jamii bora.


Naye Mwanasaikolojia Nancy Titus alisema mafunzo hayo yamemjengea uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya watu wa kada mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.


MWISHO.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi