KAMANDA WA POLISI TANGA AWATAKA BODABODA WALIOPATA LESENI KUWA MABALOZI WA USALAMA BARABARANI

 


Na Rebeca Duwe | Tanga


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amewataka vijana wa bodaboda waliohitimu mafunzo ya udereva na kupata leseni kuwa mabalozi wa usalama barabarani kwa kuwahamasisha wenzao ambao bado wanaendesha pikipiki bila leseni kujitokeza kupata elimu na kufuata sheria za barabarani.


Wito huo umetolewa wakati wa hafla ya kukabidhi leseni za udereva kwa vijana 42 waliofanikiwa kukamilisha mafunzo katika Chuo cha Udereva cha Bandiwe, yaliyofadhiliwa na Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga.


Akizungumza katika hafla hiyo, Kamanda Mchunguzi amesema vijana hao wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko katika sekta ya usafiri wa bodaboda kwa kuwa mfano bora kwa wenzao, hususan wale ambao bado wanaendesha vyombo vya moto bila kuwa na leseni.


Amesema kuendesha pikipiki bila kuwa na leseni ni hatari kwa dereva mwenyewe na watumiaji wengine wa barabara, hivyo ni muhimu madereva kupata mafunzo yanayowawezesha kuelewa sheria na kanuni za usalama barabarani kabla ya kutumia vyombo hivyo.


Aidha, amewapongeza vijana waliohitimu mafunzo hayo na kuwataka kutumia vyema fursa waliyoipata kwa kuzingatia sheria za barabarani na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.


VIJANA 42 WAPATA LESENI KATI YA 100 WALIOPANGWA


Awali, akisoma risala katika hafla hiyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Willy Mwamasika, amesema mpango huo ulilenga kuwafikia vijana 100 kutoka katika kata 11 za Halmashauri ya Jiji la Tanga.


Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali, vijana 78 ndio waliofanikiwa kufikishwa katika Chuo cha Udereva cha Bandiwe, huku vijana 42 pekee wakifanikiwa kukamilisha mafunzo na kupata leseni za udereva.


Mwamasika amesema Kamati ya Usalama Barabarani imejipanga kuendelea kuwafikia madereva wa bodaboda kwa kuwapatia elimu ya usalama barabarani na kuwawezesha kupata leseni, ili kuongeza uelewa wao kuhusu sheria na matumizi sahihi ya barabara.


Ameeleza kuwa katika kufanikisha mpango huo, Baraza la Usalama Barabarani chini ya Mwenyekiti wake, Rashid Liemba, liligharamia ada za mafunzo, leseni za muda, gharama za majaribio ya udereva (test fee) pamoja na gharama za kukata leseni za udereva zilizokuwa Shilingi 70,000.


Aidha, amesema walijisajili wanafunzi wengine 43 kwa lengo la kuongeza idadi ya vijana watakaonufaika na mpango huo, lakini nao walikumbwa na changamoto mbalimbali zilizowafanya baadhi yao kushindwa kukamilisha safari ya mafunzo.


LIEMBA: VIJANA WASIPOTEZE FURSA ZA MAFUNZO


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Rashid Liemba, amewataka vijana waliopata fursa hiyo kuwa mabalozi kwa wenzao ambao bado hawajapata nafasi ya kupata elimu ya udereva na usalama barabarani.


Liemba amesema vijana wanapaswa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo yanayotolewa kwa ufadhili, akieleza kuwa kwa sasa wanahamasishwa na kubembelezwa kutumia fursa hiyo, lakini ipo siku wanaweza kujikuta wao ndio wanaotafuta fursa hizo bila kuzipata.


Amewahimiza vijana kujitokeza na kutumia fursa zinazotolewa ili kujiongezea ujuzi na kujikinga na hatari zinazoweza kusababishwa na uendeshaji usiozingatia sheria.


BODABODA: ELIMU IMENIBADILISHA


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodaboda Kituo Na. 300, Tairi Tatu, Omari Ally Alhaji, ameishukuru Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga kwa kuwapatia fursa ya kupata mafunzo hadi kufikia hatua ya kukabidhiwa leseni za udereva.


Alisema mafunzo hayo yamemfungua macho na kumsaidia kutambua umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani, akieleza kuwa awali alikuwa akiendesha pikipiki bila kuwa na uelewa wa kutosha na kila alipomuona askari alikuwa akikimbia.


Ameongeza kuwa baada ya kupata elimu hiyo, sasa anatambua umuhimu wa kuwa dereva anayezingatia sheria na kulinda maisha yake pamoja na watumiaji wengine wa barabara.


Mafunzo hayo yanatajwa kuwa sehemu ya juhudi za Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga katika kuongeza uelewa wa madereva wa bodaboda na kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika kupitia elimu, nidhamu na uzingatiaji wa sheria za barabarani.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi