WAKRISTO WATAKIWA KUPANDA MBEGU ZA BARAKA ILI KUVUNA MAVUNO YENYE KUMTUKUZA MUNGU

 


Na Rebeca Duwe Tanga .


Wakristo wametakiwa kuwa na moyo wa kupanda mbegu za baraka katika maisha yao kwa kumtolea Mungu sadaka mbalimbali, ili waweze kuvuna mavuno yatakayowasaidia kuendelea kumtukuza na kumbariki Mungu.


Wito huo umetolewa na Mchungaji Issai Martin Mweta kutoka KKKT Usharika wa Makorora, Jimbo la Pwani, alipokuwa Mgeni Rasmi katika ibada ya Sikukuu ya Mavuno iliyofanyika katika Usharika wa Kana jijini Tanga, Jumapili iliyopita.


Akizungumza katika ibada hiyo, Mchungaji Mweta alisema kuwa mkristo anapaswa kutambua umuhimu wa kumtolea Mungu kwa moyo wa upendo na utii, akieleza kuwa kadiri anavyombariki Mungu kupitia matoleo yake, ndivyo anavyopaswa kumtegemea Mungu katika maisha yake.


Alisisitiza kuwa hakuna mavuno yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa hatua ya kwanza ya kupanda mbegu, hivyo kuwataka waumini kuwa na utamaduni wa kupanda mbegu madhabahuni ili waweze kuvuna matunda ya baraka katika maisha yao.


Akifafanua zaidi, alirejea kitabu cha Mwanzo 26:12–18, kinachoeleza namna Isaka alivyopanda mbegu na kuvuna kwa wingi. Alisema mfano huo unaonesha umuhimu wa imani, utii na kumtegemea Mungu katika kila hatua ya maisha.


Aliongeza kuwa Isaka, akiwa mwana wa Abrahamu ambaye anajulikana kama baba wa imani, alijifunza kumtii na kumsikiliza Mungu, jambo lililokuwa sehemu muhimu ya safari yake ya baraka.


Aidha, aliwakumbusha wakristo kuwa wapo wanaoweza kusikia sauti ya Mungu ndani yao lakini wakashindwa kutekeleza maelekezo yake. Hivyo, aliwahimiza kutii mwongozo wa Mungu, iwe katika kumtolea sadaka au kutekeleza mambo mengine yanayohusu imani yao, ili Mungu aonekane katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa Abrahamu.


Mchungaji Mweta alieleza pia kuwa mavuno yanahusisha kupanda mbegu na baadaye kuvuna mazao yanayozidi mbegu zilizopandwa. Hivyo, aliwataka waumini kuwa na moyo wa kumtolea Mungu kwa upendo na shukrani wanapopokea baraka zake.


Alisema Mungu ndiye mwenye hekima kuu katika masuala ya uchumi na ndiye chanzo cha mafanikio ya mwanadamu. Kwa msingi huo, aliwakumbusha wakristo kutomsahau Mungu wanapofanikiwa na kupata mali, akirejelea kitabu cha Kumbukumbu la Torati 8:12.


Kwa upande wake, Mkuu wa Jimbo la Pwani ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kana jijini Tanga, Mchungaji Issai Amasia Mweta, aliwahimiza wakristo kuwa na moyo wa kumbariki Mungu kwa kutambua kuwa wanapaswa kumtegemea katika kila jambo la maisha yao.


Mchungaji Amasia Mweta aliwataka waumini kuachana na tabia ya kuwaonea wengine wivu wanapofanikiwa au kubarikiwa, badala yake kila mmoja ajitathmini na kutafuta namna ya kufikia mafanikio hayo kwa njia inayompendeza Mungu.


Aidha, aliwakumbusha wakristo umuhimu wa kutoa sadaka kwa moyo wa kujitoa, akieleza kuwa sadaka yenye thamani kwa mtoaji inapaswa kuambatana na moyo wa kujitolea na upendo wa dhati kwa Mungu.


Alisisitiza kuwa waumini wanapaswa kuwa na moyo wa utoaji unaoonesha imani yao na kuthamini nafasi ya Mungu katika maisha yao.


MWISHO.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi