LICHA ya Serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
kutoa elimu ya kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango kote nchini, baadhi ya
wanawake katika wilaya ya Mbeya Vijijini na Jiji la Mbeya wamekuwa wakitumia
majivu kama njia ya kupanga uzazi na kutoa
mimba zisizotarajiwa.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala hii katika mji
wa Mbalizi Mbeya Vijijini na kata ya Manga na Foresti Jijini Mbeya umebaini
kuwa wanaoongoza kwa kutumia njia hiyo ni pamoja na wake za watu na wahudumu wa
Bar.
Wanawake waliohojiwa wakiwemo wawili kati yao ambao wakawa na mahusiano na mwandishi wa
makala haya ili kukamilisha uchunguzi, walisema kuwa majivu hayo wanakunywa
kikombe kimoja kila baada ya kumaliza kufanya tendo la ndoa na wanaume ambao
wana mahusiano nao ya kimapenzi na wengine waume zao.
‘’Majivu unatakiwa unywe ndani ya masaa 12 baada ya kutoka
kufanya tendo la ndoa ili mimba isitunge’’ anasema Mama Angel mkazi wa eneo la
Mama John ambaye ni mke wa mtu.
Mama Angel anakiri kuwa amewahi kutoa mimba kwa njia za
kisasa ambayo haikuwa mimba ya mumewe na alipoambiwa kuwa kuna njia zingine za
kujikinga ikiwemo kunywa majivu baada ya tendo la ndoa ameendelea kutumia njia
hiyo kwa miaka mitatu sasa.
‘’Kule hospitali nilitundikiwa maji ya uchungu ambayo
yanaongeza njia na ndani ya masaa matatu mimba ikatoka’’ anasema Mama Angel
bila kutaja hospitali aliyotolea mimba.
Uchunguzi huo uliofanywa mwezi Octoba na Novemba 2012,
umebaini kuwa kwa sasa wanawake wengi hawapendi kutumia njia za uzazi wa mpango
wa kisasa mfano Sindano, vipandikizi na vidonge kwa madai kuwa huduma hizo zina
madhara.
Wanawake 43 waliohojiwa wakiwemo wake za watu 13 walisema
kuwa madhara waliyoyapata baada ya kutumia njia za uzazi wa mpango wa kisasa ni
pamoja na kupoteza hamu ya kufanya tendo la ndoa.
Baadhi walisema kuwa wanaogopa kufanyiwa upasuaji
(kusafishwa) kunakotokana na uvimbe unaosadikika kutokea baada ya kutumia kwa
muda mrefu huduma hizo za kisasa hasa vidonge maarufu kama
majira.
‘’Tarehe za Hedhi hubadilika na kutoeleweka baada ya kutumia
dawa hizo za uzazi wa mpango wa kisasa zikiwemo sindano na vidonge’’ anasema
Naomi Haule ambaye ni mhudumu wa Bar.
Wengine ambao waliomba hifadhi ya majina yao, wanasema mbali
na kutumia majivu kama njia ya uzazi wa mpango kuzuia mimba na utoaji mimba,
baadhi yao wanatumia kisamvu, Vidonge vya uzazi wa mpango maarufu kama (Majira)
na majani ya mti unaojulikana kwa jina la Songwa kutoa mimba zisizotarajiwa.
‘’Wake za watu wanaopata mimba ambazo si za waume wao,
wafanyabiashara na wahudumu wa Bar siyo siri tunaongoza katika kutumia njia
hizi na utoaji mimba kwa njia za kienyeji’’ anasema Rehema Mwakitalu akiwa na
wenzake eneo la Mwanjelwa ambaye pia ni muhudumu wa Bar.
Walipoulizwa kuwa kwanini wasitumie njia za kisasa katika
utoaji mimba walisema kuwa kikwazo ni gharama za utoaji mimba kwa njia za
kisasa ambapo mwanamke mwenye mimba ya mwezi mmoja hutozwa Shilingi 40,000 ili
asaidiwe kutoa mimba hiyo.
Walizitaja hospitali ambazo zinahusika kutoa mimba hizo kwa
siri kuwa ni pamoja na hospitali ya wazazi Meta
na zahanati zingine za madaktari binafsi zilizopo eneo la Nzovwe, Mama John na
Uyole.
Aidha mbali na hospitali hizo, wanawake hao walisema kuwa
pia kuna waganga na wakunga wa jadi wanaowasaidia kutoa mimba hizo ambazo
wanadai kuwa hazikutarajiwa na kwamba wakunga hao wapo eneo la Mapelele wilaya
ya Mbeya na Iwambi Jijini Mbeya.
Kuhusu maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi wanasema; ‘’ Ni bora
kupata ukimwi kuliko mimba kwasababu ukipata ukimwi unajulikana baada ya mud
asana na unapata dawa za kurefusha maisha lakini mimba ukipata huwezi kuendelea
na starehe na ukijifungua unalazimika kulea mtoto kwa muda mrefu huku na
wanaume wengi hawaeleweki kwenye matunzo’’ wanasema wanawake hao.
Wanawake wahudumu wa Bar walipoulizwa kuwa kwanini wanatumia
zaidi majivu kama njia ya uzazi wa Mpango na utoaji Mimba walisema kuwa baadhi
ya wanaume huwa hawapendi kutumia mipira (Condom) wakati wa kujamiiana hivyo
baada ya tendo la ndoa wanalazimika kutumia njia hiyo kama
moja ya njia rahisi ya kuzuia mimba kutotunga.
Walipoulizwa kama wanajua madhara ya kutumia huduma ya
majivu na kisamvu kwa muda mrefu kama huduma ya uzazi wa mpango na utoaji mimba
walisema kuwa hofu yao ni kwamba wanaweza kupata kansa au kutozaa tena.
‘’Ili kuepukana na kupata
madhara ya kansa yanayoweza kutokana na majivu, huwa mtu akinywa basi siku hiyo
anatakiwa kunywa maji kwa wingi ili kupunguza kemikali zitokanazo na majivu’’
anasema Asha Juma.
Anasema yeye ni Mama wa watoto watatu na tangu amepata mtoto
wake wa kwanza mwaka 1998 amekuwa akitumia majivu kila baada ya tendo la ndoa.
Na kwamba alipojaribisha kutumia vidonge alisumbuliwa na
nyonga na kukosa hamu ya tendo la ndoa hatimaye akaenda kusafishwa na alipojaribisha
sindano pia alipata madhara ya kukosa hamu ya tendo la ndoa ambapo mpaka sasa
anatumia Majivu kama njia salama kwake ya
uzazi wa mpango.
Baadhi ya madaktari waliohojiwa kwa sharti la kutoandika
majina yao
gazetini wamekiri kuhusika na biashara ya utoaji mimba kwa njia za kisasa na
kuzitaja njia wanazotumia.
‘’Wenzetu kuna sheria za utotaji mimba lakini ajabu hapa
Tanzania tunakataza wakati watu wengi wanatoa mimba tena hasa wake za watu na
njia ambazo wengi tunazitumia kwa usalama zaidi ni kuwatundikia Drip za maji ya
uchungu na vidonge vya uchungu vinavyoongeza njia kwa mwanamke’’wanasema
madaktari hao kwa nyakati tofauti.
Siku wanazotumia zaidi ni siku za Jumapili ambapo wanasema
kuwa baada ya kumaliza utoaji huo wa mimba wanawake hao wanatoka wakiwa salama
na kuwapatia dawa za kutuliza maumivu na kuwashawishi kula vyakula na vinywaji
vya kuongeza damu.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, katika sayansi ya akili watu
wanaojamiiana huwa wanatumia kinga mara ya kwanza na ya pili baada ya kuanza
mahusiano na huwa hawatumii tena kinga baada ya kukutana mara ya tatu na nne na
kuendelea.
Sanjari na hayo imebainika kuwa wauguzi wengi huwa hawatumii
njia za kisasa za uzazi wa mpango licha ya kuendelea kuwashawishi wananchi
wengine kutumia njia hizo kwa madai kuwa vidonge hivyo huwa wakimeza
haviyeyuki.
‘’Sisi wengi hatutumii kwasababu kuna madhara makubwa
ukitumia kwa muda mrefu ambapo ukitaka kuzaa unalazimika kwenda kusafishwa
kizazi na vidonge hivyo haviyeyuki na inatia hofu kuwa ukikwanguliwa unaweza
usizae tena’’ walisema baadhi ya wauguzi wa hospitali za Ifisi Mbalizi na
hospitali ya wazazi Meta kwa sharti la kutotaja majina yao .
Mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Mbeya
Prisca Butuyuyu, anasema kuwa mila na desturi ni tatizo katika utumiaji sahihi
wa uzazi wa mpango na kwamba katika wilaya ya Mbeya Vijijini mwaka 2011
vilitokea vizazi hai 38 kati ya 100,000 na vifo 113.
Kwa upande wa Jiji la Mbeya mwaka 2011 anasema vizazi
vilikuwa 109 kati ya 100,000 na vifo vilikuwa 363 ambapo katika uzazi huo
hospitali ya wazazi meta ndiyo inahusika zaidi na inahudumia wanawake pia
wanaotoka nje ya Jiji la Mbeya.