F Sekta ya utalii kutoathiriwa na kodi mpya ya VAT | Muungwana BLOG

Sekta ya utalii kutoathiriwa na kodi mpya ya VAT

Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) iliyowekwa na serikali kwenye huduma za utalii imeelezwa kuwa haitakuwa na madhara kwa ukuaji wa sekta hiyo kama ambavyo wadau wengi wa utalii wamekuwa wakisema na kuilalamikia.

Mdau wa utalii ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jumia Travel kanda ya Afrika Mashariki Bi. Estelle Verdier-Watine, amesema hayo jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na wanahabari na kufafanua kuwa bahati iliyonayo Tanzania ni utajiri wa vivutio vya utalii huku akishauri nguvu kubwa ielekezwe kwenye kuvitangaza vivutio hivyo.

Amesema kwa sasa kutakuwa na athari ndogo sana zitakazotokana na mtazamo wa kisaikolojia walionao wanadamu ila kulingana na upekee wa vivutio vya utalii ilivyonavyo Tanzania, kuna kila dalili kuwa watalii wataendelea kuja nchini kwa wingi kwa ajili ya kuja kujionea vivutio hivyo.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo hapa nchini Bi. Fatema Dharsee amesema utalii ni moja ya sekta zinazokuwa kwa kasi ulimwenguni kote na kwamba Tanzania ina kila sababu ya kufaidika na ukuaji huo kwa kuhakikisha malengo ya kufikia watalii milioni mbili wanaokuja nchini linafikiwa.