Mambo yakufanya unapokuwa na hasira


Yapo mambo kadha wa kadha ambayo hutokea katika maisha ambayo yatakufanya uwe na hasira katika maisha, inapotokea hali kama hii basi unatakiwa kufanya mambo yafuatayo:

Jifunze kukaa kimya unapokuwa na hasira.
Hii ni njia muhimu ya kuondokana na hasira pamoja na madhara yatakayo ambatana nayo. Ni jambo la busara kutokuzungumza chochote unapokuwa umekasirika. Kwa kuzungumza huku ukiwa ni mwenye hasira kunakuza majibizano, malumbano, kutokuelewana, na kufanya hali kuwa mbaya zaidi. Jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine linaweza kupeleka kuumiza hisia za wengine. Unapozungumza huku ukiwa na hasira, unakuwa unazidisha chuki na hasira kutoka kwa wengine. Lakini kama utajizuia na kukaa kimya utakuwa unaruhusu kuondoka kwa hisia za hasira.

Wapuuze wanaotafuta kukufanya uwe na hasira.
Wakati mwingine hasira zetu huwa zinachochewa na watu wengine. Kuna aina ya watu ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakitafuta kila namna ya kutaka kukufanya uwe mwenye hasira. Hawa ni watu unaopaswa kuwapuuza, na kwa kuwapuuza huko kutafanya maneno na matendo yao yasiwe na athari yoyote kwako. Na kwa kufanya hivyo,utakuwa umefaulu kudhibbiti hasira yako badala ya kuiruhusu hasira ikudhibiti.

Tafakari.
Wakati tunapohisi kupandwa na hasira ni muhmu tukajizuia na kutafakari kuhusiana na hasira zetu kwa kujinenea wenyewe. Unaweza ukajiambia “Hasira hii haitonisaidia kwa namna yoyote.Hasira hii itafanya hali kuwa mbaya zaidi”. Hata kama sehemu fulani ndani yetu itabakai kuwa na hasira, lakini kwa kujinenea maneno hayo kutatusaidia katika kutuweka mbali na hisia za hasira.

Thamini amani kuliko hasira.
Hali yetu ya kutokuwa wakamilifu inafanya iwe vigumu zaidi kwetu kuepuka hasira na matendo ya hasira.Lakini licha ya hivyo yatupasa kutambua kwamba; hasira isiyodhibitika inaweza kutufanya tufanye mambo ambayo tutakuja kuyajutia baadaye. Kuwa na hasira ni jambo la kawaida, ila ni muhimu tukajifunza kuthamini amani kuliko hasira. Na hii itatusaidia katika kuondokana na hasira.

Kazia fikra zako kwenye mambo mengine.
Njia nyingine ya kuondokana na hasira ni kwa kubadilisha umakini wako. Hapa unakuwa unahamisha fikra zako kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, kutoka fikra hasi kwenda fikra chanya.Kwa mfano;tuseme fulani amefanya jambo fulani ambalo linapeleka wewe kuwa na hasira, basi unachotakiwa kufanya hapo ni kufikiria kitu kingine ambacho kitakufanya uwe mwenye furaha.Tiba pekee ya mawazo hasi ni mawazo chanya.

Jaribu kuwaelewa walio karibu yako.
Moja ya ujuzi muhimu ambao kila mmoja wetu anapaswa kujifunza ni ule ujuzi wa kuwaelewa wengine. Huu ni ujuzi wenye nguvu na wenye mchango mkubwa sana kwa mafanikio yako katika maisha na biashara.Na ujuzi huu unaanzia kwa kujielewa mwenyewe,na kisha ndo uweze kuwaelewa wengine.Kwa kufahamu hulka au tabia za wengine kwa namna moja ama nyingine kutakusaidia sana katika kuondokana na hasira. Kwa kuwaelewa wengine itakusaidia kufahamu ni kwanini wengine wanatenda au kufanya kile wanachofanya.

Tabasamu.
Njia nyingine na iliyo rahisi ya kuondokana na hasira ni kutabasamu. Hakuna kitu chenye nguvu kama tabasamu. Tabasamu halikugharimu chochote. Unapokuwa unatabasamu unakuwa unaondoa na kufuta hisia zote zilizo hasi ikiwemo hasira.