Wanajeshi wa Afghanistan wamuuwa afisa wa ngazi za juu wa kundi la IS

Idara ya ujasusi nchini Afghanistan imesema kuwa imemuuwa Assadullah Orakzai, afisa mmoja wa ngazi za juu wa kundi linalojiita dola la kiislamu, IS wakati wa operesheni moja Kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na makao makuu ya kitaifa ya ulinzi hapo jana jioni, imesema kuwa Orakzai alikuwa kiongozi wa kijasusi kwa kundi hilo la IS na vikosi maalumu vya kijeshi vilimuuwa karibu na mji wa Jalalabad. Orakzai alishukiwa kuhusika katika mashambulizi kadhaa hatari dhidi ya jeshi na raia nchini humo.

Wiki iliyopita, ripoti moja ya Umoja wa Mataifa, ilisema kuwa Afghanistan imeshuhudia kupungua kwa asilimia 13 ya idadi ya raia waliouawa na kujeruhiwa katika ghasia kote nchini humo katika muda wa miezi sita ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka jana.

Ripoti hiyo ilisema hatua hiyo inatokana na operesheni ya kupunguzwa kwa vikosi vya kigeni ambavyo kwasasa huchukuwa hatua tu vinapohitajika kutoa usaidizi kwa vikosi vya serikali ya Afghanistan na pia kupungua kwa idadi ya mashambulizi yanafanywa na kundi la wanamgambo la IS.