Aug 2, 2020

Wasimamizi wa uchaguzi mkoani Tabora waonywa

  Muungwana Blog 2       Aug 2, 2020
WARATIBU wa Uchaguzi wa Mikoa na Wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu ngazi ya Wilaya na Majimbo wameonywa kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kutakiwa kuzingatia matakwa ya Katiba,Sheria na kanuni zinazosimamia zoezi la Uchaguzi ili kutosababisha malalamiko.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora Afisa Sheria kutoka  Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC)  Athuman Kimia wakati wa Mafunzo kwa wasimamizi hao wa uchaguzi 110 toka mikoa na Kigoma na Tabora.

Alisema lengo la kutoa mafunzo hayo kwa Waratibu na wasimamizi ni kutaka wasimamie uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu uwe huru, wa haki na kuaminika .

Kimia aliwataka wazingatie viapo vyao kwani vinawataka watende majukumu yao kwa mujibu wa Sheria na endapo watakiuka watakuwa wametenda kosa la jinai na hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi zinavyoelekeza.

Alibainisha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaowajibu wa kutoa mafunzo yanayolenga taratibu za kuendesha uchaguzi kwa Waratibu wa Mikoa, Wasimamizi wa ngazi zote wakiwemo wa Wilaya,Majimbo,Vituo pamoja na Maafisa Ugavi.

Awali akifungua mafunzo hayo Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Hassan Mwandobo alisema kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yanalenga namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za Uchaguzi.

Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo watambue kuwa wameaminiwa kufanya kazi hiyo hivyo ni muhimu wakajiamini na kutambua kwamba wanapaswa kuzingatia kanuni za uchaguzi, Maadili yake na Maelekezo yatakayotolewa na Tume.

Mwandobo aliwataka Waratibu wa Mikoa, Wasimamizi wa ngazi zote wakiwemo wa Wilaya,Majimbo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao wavishirikishe vyama vya siasa pamoja na wadau wengine wakiwemo viongozi wa dini.
logoblog

Thanks for reading Wasimamizi wa uchaguzi mkoani Tabora waonywa

Previous
« Prev Post