Asakwa na Jeshi la polisi kwa kusababisha kifo cha mke wake na kumtelekeza hospitali


Na John Walter-Manyara

Mtu mmoja anayefahamika kwa majina ya Doh  Hamsii Kodi mkazi wa Kijiji Cha Gidas wilaya ya Babati Mkoani Manyara anatafutwa na Jeshi la polisi kwa kosa la kumuua mke wake na kumtelekeza akiwa hospitali baada ya mwanamke huyo kufariki alipopelekwa kwa ajili ya matibabu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa jeshi la polisi Mkoani hapa Paul Kasabago  alisema marehem alikuwa akifahamika kwa majina ya Juliana Ironga Gadie mwenye umri wa miaka 45 na alipigwa na Mume wake ambaye anafahamika kwa majina ya Doh Hamsii Kodi ambaye amekuwa akimlaumu mara nyingi marehem kwa kushindwa kuwa mwaminifu kwenye ndoa yao.

"Chanzo cha tukio ni  wivu wa mapenzi kutokana na mme wa marehem amekuwa akimtuhumu mara kwa mara mke wake kwa kutokuwa mwaminifu kwenye ndoa ndipo alipoamua kumpiga mke wake na kitu butu kichwani hali iliyosababisha kupata maumivu makali"alisema Kamanda.

Kamanda alisema kuwa mtuhumiwa alipoona marehem kazidiwa alimchukua na kumpeleka zahanati ya kijiji cha Gidas ambapo baada ya kufika hapo kutokana na hali ya marehem kuwa mbaya alifariki kabla ya kupata matibabu.

"Mume wake ambaye ni mtuhumiwa alipobaini mke wake amefariki alichofanya ni kumwambia nesi ngoja niende hapo mnadani nikawaite ndugu zake na marehem kutokana  na siku hiyo ilikuwa siku ya mnada wa Gidas ndipo alipochukua usafiri wa bodaboda na kuelekea huko alipodang'anya anaenda kuwatafuta ndugu wa mke wake ambapo hakurudi mpaka leo,hivyo tunaendelea kumtafuta"aliongeza.

Kamanda alisema baada ya kufanya uchunguzi  wataalam wa hospitalini hapo waligundua kwamba pamoja na marehem kupigwa na kitu kibutu kichwani lakini pia alinyongwa.

Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na serikali ya kijiji bado wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa mahakamani na kujibu mashitaka yake.

Ata hivyo kamanda amewasihi wananchi Mkoani hapo kutokuchukua sheria mkononi pale inapotokea kutokuelewana kwani kuna sheria na taratibu ambazo zimewekwa kwa ajili ya kuwasaidia ikiwemo mahakama ambazo zinaweza kuwaachanisha endapo itatokea kutokuelewana.

Alisema kuchukua sheria mkononi ni uhalifu hivyo jamii inatakiwa kurudi kwenye maadili mazuri ambayo yatasaidia kupunguza vitendo viovu.

Post a Comment

0 Comments