Jan 14, 2021

Mamia ya Wastaafu wanaolipwa pensheni na Hazina wahakikiwa kanda ya Ziwa

MAMIA ya wazee wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina), wamejitokeza kuhakikiwa katika Mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita, ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuhuisha taarifa za wastaafu hao.


Akizungumza Jijini Mwanza, Mratibu wa zoezi hilo ambaye pia ni Mhasibu Mkuu sehemu ya pensheni kutoka Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Scola Mafumba, amesema kuwa uhakiki huo umelenga kuhuisha taarifa za wastaafu hao na kuziweka kwenye mfumo wa kieletroniki.

Alieleza kuwa zoezi hilo lilianza rasmi tarehe 7 Desemba mwaka 2020 na linatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka 2021 ambapo mpaka sasa wazee wastaafu katika mikoa 10 ya Tanzania bara wamehakikiwa na kwamba zoezi hilo litafanyika hadi Zanzibar.

“Baada ya hapa tutaelekea mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu kuanzia tarehe 18 Januari, 2021 ambapo kazi tunayoifanya ni kuhakiki na kukusanya taarifa za wastaafu na kuziweka kitaalam ili kuboresha kanzidata ya wastaafu iliyoko Hazina” aliongeza Bi. Mafumba

Alisema kwamba zoezi hilo ni la lazima kwa wastaafu wote na kuongeza kuwa Wastaafu ambao hawatahakikiwa wataondolewa kwenye orodha ya malipo ya Pensheni kuanzia Aprili, 2021


Aidha, Bi. Mafumba aliwaasa wastaafu kujiepusha ama kujihadhari na matapeli wanaowarubuni kwamba watawasaidia kupata pensheni zao na kuwadai rushwa ambapo amesema huduma za wastaafu zinatolewa bure na Serikali.

“Kama kuna mstaafu anataka kupata taarifa zozote zinazohusu mafao yao tunawashauri wafike kwenye ofisi za Hazina Ndogo zilizoko mikoa yote nchini na kamwe wasikubali kutoa fedha zao kwa mtu yeyote kwa sababu huduma za wastaafu zinatolewa bure na Serikali” Alisisitiza Bi. Mafumba.

Kwa upande wao, Wazee Wastaafu wameipongeza Serikali kwa hatua wanayochukua ya kuwahakiki na kuboresha taarifa zao ambazo zitakuwa zikipatikana mahali popote kwa njia ya mtandao.

Aidha, wameiomba Serikali kuwaongezea pensheni wanayolipwa kila mwezi ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha zinazowakabili ikiwemo afya.

 

KWA HABARI ZAIDI <DOWNLOAD HAPA>
Share:
Loading...

Popular Posts

Copyright © MUUNGWANA BLOG | Powered by Blogger