Marekani kuanza tena kufadhili WHO


Marekani itaanza tena kufadhili Shirika la WHO na kujiunga katika ushirika unaolenga kugawanya chanjo ya virusi vya corona kote ulimwenguni huku rais Joe Biden akitilia mkazo sheria za kuzuia maambukizi ya virusi hivyo

Hatua hiyo iliyotangazwa jana na mshauri mkuu wa rais Joe Biden kuhusiana na janga la virusi vya corona Dkt Anthony Fauci, inafufua upya uungwaji mkono wa shirika ambalo uongozi wa Trump ulijitenga nalo. Kujitolea haraka kwa Dkt Fauci kwa shirika hilo la WHO ambalo mikakati yake ya kushugulikia janga la virusi vya corona ilikosolewa na wengi, lakini zaidi na utawala wa Trump, kunaashiriamabadiliko katika hatua ya ushirikiano zaidi katika kukabiliana na janga hilo.

Dkt Fauci ameongeza kusema kwamba anafurahia kutangaza kwamba Marekani itabaki kuwa mwanachama wa Shirika la afya duniani na kwamba rais Biden alitia saini barua zinazoondoa tangazo la awali la utawala wa Trump kujiondoa katika shirika hilo. Hili ni tangazo la kwanza la umma la afisa wa serikali ya Biden kwa hadhira ya kimataifa na ishara ya kipaombele ambacho rais huyo mpya ametoa katika vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 nchini humo pamoja na washirika wa kimataifa.

Wakati huo huo, Akitia saini maagizo 10 ya rais katika ikulu ya White House, Biden ameliambia taifa hilo kwamba idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 huenda ikaongezeka hadi nusu milioni kufikia mwezi ujao na kwamba hatua za dharura zinahitajika. Biden amesema kuwa taifa hilo liko katika hali ya dharura na ni wakati wa kuichukulia hali nchini humo kuwa hivyo.

Ameongeza kwamba anataka kurejesha imani ya umma baada ya utawala wa mgawanyiko wa Donald Trump. Biden amesema chini ya utawala wake, wanasayansi watafanya kazi bila kuingiliwa kisiasa na kuahidi kushauriana nao kila wanapokosea. Maagizo mengine ya Biden yalijumuisha kutilia mkazo mpango wa chanjo ambao bado unayumbayumba na kusisitiza kuvaa barakoa katika uchukuzi wa umma.

Ijapokuwa chanjo zilitolewa kwa kasi ya juu katika mwaka wa mwisho wa uongozi wa Trump, mchakato wa kutolewa kwake umekumbwa na changamoto nyingi. Biden ametangaza lengo la kutolewa kwa chanjo milioni 100 katika siku 100 huku wataalamu wake wakuu wakisema hatua hiyo inawezekana. Kufikia sasa ni vipimo milioni 16.5 pekee vya chanjo vilivyotolewa .


 

Post a Comment

0 Comments