Pompeo: Iran ni 'kambi mpya' ya mtandao wa magaidi wa al-Qaeda


Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ameilaumu hadharani serikali ya Iran kwa kuruhusu mtandao wa kijihadi wa al-Qaeda kubuni "makao mapya makuu " nchini humo.

"Tofauti na Afghanistan, ambako al-Qaeda ilikuwa inajificha milimani, leo hii kundi la al-Qaeda linafanya kazi chini ya ulinzi wa utawala wa Iran," aliambia shirika la wanahabari la National Press Club.

Mwezi Novemba mwaka jana, Iran ilipinga ripoti kwamba naibu wa kamanda wa al-Qaeda Abdullah Ahmed Abdullah, anayefahamika pia kwa jina la Abu Muhammad al-Masri, alipigwa risasi na kuuawa mjini Tehran na maajenti wa Israeli, kufuatia ombi la Marekani.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington siku ya Jumanne, Bw. Pompeo alisema anaweza kuthibitisha kwa mara ya kwanza kwamba Masri alifariki Agosti 7, japo hakutoa maelezo zaidi.

Alisisiza kwamba ni makosa kuamini uongozi wa madhehebu ya Waislamu wa Kishia (Iran) na Kikundi cha Sunni ambacho kinachukulia Washia kuwa wazushi na maadui wakubwa.

"Uwepo wa Masri ndani ya Iran unaashiria sababu ya kwanini tuko hapa leo. Al-Qaeda imepata makao mapya : Ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

"Kutokana na hilo, kundi baya lililobuniwa na [Osama] Bin Laden linaelekea kupata nguvu na uwezo."

Tangu mwaka 2015, Bw. Pompeo amekuwa akidai kwamba, Tehran imeruhusu viongozi wa al-Qaeda nchini humo kuwa huru kuwasiliana na wanachama wengine na kutekeleza majukumu mengine ambayo yalikuwa yakiendeshwa kutoka Afghanistan na Pakistan, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha mashambulio, propaganda, na kuchangisha fedha.

"Uwepo wa al-Qaeda ndani ya Iran unatishia usalama wa mataifa na hata ndani Marekani kwenyewe," aliongeza.

Waziri huyo wa Mambo ya nje pia alisema Marekani ilikusudia kutoa hadhi ya Magaidi Maalum Walioteuliwa Ulimwenguni kwa viongozi wawili wa al-Qaeda ambao iliamini kuwa walikuwa nchini Iran: Mohammed Abbatay, ambaye pia anafahamika kama Abdul Rahman al-Maghrebi, na Sultan Youssef Hassan al-Arif.

Post a Comment

0 Comments