Wavuvi wafikishiwa elimu ya uzazi wa mpango


Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dk.Angelina Mabula amesema serikali imeanza kuchukua hatua kufikisha elimu ya uzazi wa mpango kwenye maeneo ya visiwani yanayokaliwa na wavuvi, ambapo kila mwezi timu ya wataalamu wa afya huwafikia ili kuwaelimisha namna bora ya kuzaa na kulea watoto.

Dk.Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, amesema hatua hiyo inakuja baada ya kubainika ongezeko la msongamano watu wazima na watoto kwenye maeneo ya visiwani ikiwemo kisiwa cha Kome hali inayoweza pelekea changamoto za huduma za kijamii.

Amesema katika kipindi hiki ni vyema wazazi wakajenga utamaduni wa kuweka mipango ya namna ya malezi kwani uwepo wa watoto wengi ndani ya familia bila namna nzuri ya malezi inaweza kuchangia changamoto za huduma bora kwa watoto.

"Tayari serikali inachukua hatua, na huku wilayani kwangu kuna huduma ya mikoba inakwenda visiwani, kina mama wanakuja kliniki wanaambiwa habari ya uzazi wa mpango, wanaelimishwa juu ya lishe bora, na wanaambiwa namna ya kupangilia vizuri ili waweze kulea watoto na kuwasomesha vizuri.

"Jambo ambalo lipo ni kwamba huku visiwani wengi wanakaa kwenye makambi, ambapo zoezi la uvuaji samaki linafanyika jioni, kuanzia mida ya saa tisa wakirudi kutwa nzima wamelala, wanakusanya nguvu kwa ajili ya kwenda kufanya kazi.

"Kwa hiyo unakuta wanapata muda mwingi zaidi wa kuwa nyumbani na wenzi wao na hivyo kuzaliana kunakuwepo kwa namna hiyo na ndiyo maana leo hii tunashuhudia ongezeko la watu kama hivi," amesema Dk.Mabula

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima, amesema hatua ya kufikisha elimu ya afya ya uzazi maeneo ya visiwani inakusudia kuongeza uzazi salama kwa kina mama sambamba na kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani jijini Mwanza.

Post a Comment

0 Comments