ADEM Bagamoyo yawanoa vikali Walimu wapatao 284 wa Shule za msingi mkoa wa Pwani juu ya uthibiti ubora


Na Victor Masangu, Bagamoyo.

AFISA  Elimu wa Mkoa wa Pwani Hadija Mcheka amesema ni lazima Walimu Wakuu watambue wajibu wao wa kuhakikisha wanatekeleza  shughuli ipasavyo katika suala zima la utoaji wa elimu katika shule za Msingi, zinatekelezwa kikamilifu ili  watoto waweze kupata elimu bora na si bora elimu na kuzalisha wahitimu wenye maarifa.

Mcheka ameyabainisha hayo  mjini Bagamoyo wakati akifunga Mafunzo maalum ya Uthibiti Ubora wa Shule wa ndani kwa Walimu wakuu 284 kutoka Mkoa wa Pwani yaliyofanyika Katika Tasisi ya Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) 

Alisema mafunzo hayo yamewaongezea umahiri katika uongozi, kusimamia, kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kutoa huduma ya elimu vile inavyopaswakwa kufuata   miongozo inayotolewa na kwamba  pamoja na miongozo hiyo bado yamekuwa yakihitaji kupata mafunzo kama hayo ili kuboresha utendaji kazi. 

 Mcheka alisema, nia ya Serikali  ni kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu katika taasisi za elimu ikiwemo Shule za Msingi kama ilivyofanya. 


Aliwakumbusha walimu Wakuu wa Mkoa wa huo kwenda kuyafanyia kazi maeneo yote ambayo yamefundishwa katika siku za mafunzo, huku akisisitiza kutumia mafunzo hayo katika kuimarisha uongozi na ufundishaji  kwani kwasasa unahitajika Uongozi bora unaoleta matokeo chanya na Uongozi unaoacha alama katika sekta ya Elimu hapa nchini.

"Mkoa utaendelea kuitumia ADEM katika mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa elimu na kufanya ufuatiliaji katika Shule za Msingi kuona kama Walimu Wakuu waliopokea mafunzo haya wanayatumia kuleta mabadiliko na matokeo chanya katika maeneo yao" alisema.


Nae Kaimu Mtendaji mkuu wa wakala wa Maendeleo ya Elimu (ADEM), Dkt. Alphonce Amuli aliwashukuru walimu hao walioitikia wito wa kuhudhuria mafunzo hayo na kuwataka kuyatumia kama chachu ya kwenda kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa utolewaji wa elimu bora katika vituo vyao.

Alisema mafunzo hayo ya Uthibiti Ubora wa ndani wa Shule kwa walimu wakuu, yamefadhiliwa na mradi wa GPE-LANES II  na kuratibiwa na kuendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) ambapo katika awamu ya pili ya utoaji wa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa Walimu Wakuu 284 katika Mkoa wa Pwani, 210 kutoka Mkoa wa Songwe na 196 kutoka Mkoa wa Dar Es Salaama.

Alibainisha kuwa awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yamefaanyika Mwezi Januari kwa kutoa mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa ndani kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 8,091 wa Tanzania bara..

 

Post a Comment

0 Comments