Bwege: Wapinzani tusijaribu kumzingua Rais

 


Na Ahmad Mmow, Lindi. 

Viongozi wa vyama vya upinzani vya siasa nchini wametahadharishwa wasimuamrishe Rais afanye wanayotaka. 

Wito na tahadhari hiyo imetolewa na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini, Seleman Bungara (Bwege) leo alipozungumza na Muungwana Blog kwa simu kutoka Kilwa Kivinje. 

Alisema kuna dalili kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kutaka kumshinikiza Rais badala ya kumuomba na kushauri afanye wanayotaka wao. 

Bwege alisema wapinzani hawana haki wala sababu ya kumshinikiza Rais Samia Suluhu Hassan. Bali wamshauri, wamshawishi na wamuombe afanye ambayo wanadhani yana tija kwa taifa.

Bila kuwataja   viongozi hao, alisema wanamshinikiza Rais Mama Samia Suluhu Hassani badala ya kumkumbusha,  Kumshawishi na kumuomba. 

Huku wakijua kwamba Rais hashinikizwi, bali anauoneshwa ukweli na kuambiwa kiustarabu na heshima.

Alisema wapinzani wanatakiwa watambue ukweli kwamba  Rais ni kama mtu aliyeshika mpini wakati wapinzani ni kama mtu alishika kisu kwenye makali. 

 ''Hekima inahitajika. Tukimzingua, atatuzingua na hatutakuwa na uwezo wowote wa kumzuia. Tutakuwa hatuna la kumfanya. 

Kada huyo wa chama cha ACT-Wazalendo aliweka wazi kwamba uwezo huo Rais anao bali  awe hajaamua tu.

Mbunge huyo wa zamani ambae katika kipindi chake alikuwa kivutio ndani ya ukumbi wa bunge kwa mtindo wa uwasilishaji na ujengaji  hoja zake alisema Rais Mama Samia Suluhu Hassani ni wa kukumbushwa, Kushauriwa, kuambiwa na kuombwa. 

Kwani  mengi mazuri na mabaya anayajua. Naiwapo kuna ambayo hayajui akumbushwe, ashauriwe na kuombwa kwa busara na hekima badala ya kumshinikiza. 

 '' Lazima tukubali kwamba  yeye ndiye Rais kwa mujibu wa Katiba yetu. Natukumbuke kwamba mwaka 2020 alizunguka kuomba kura. 

Tulipompigia kura mtangulizi wake maana yake na yeye tulimpigia. Kwamaana hiyo tulimchagua,'' Bwege alisisiza. 

Aidha Bwege aliweka wazi kwamba  kumkosoa Rais siyo dhambi na watakao mkosoa wasionekane kama hawampendi au wana nongwa. 

Bali ukosoaji uwe wenye tija kwa taifa na washauri nini kifanyike. Bali ukosoaji huo usiwe na dhamira ya kutafuta mitaji ya kisiasa zaidi badala ya masilahi ya nchi. 

Post a Comment

0 Comments