Hatua kali kuchukuliwa kwa waliokamatwa na shehena ya vifungashio vilivyopigwa marufuku

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo ameagiza kuchukuliwa hatua kali kwa watu waliokamatwa na shehena ya vifungashio vilivyopigwa marufuku na Serikali.

Jafo ametoa kauli hiyo jana baada ya kushuhudia maguni 40 na katoni 16 za vifungashio hivyo ambavyo havina ubora vilivyokamatwa wakati wa msako uliofanywa soko kuu katika Jiji la Mwanza.



Akizungumza baada ya kushuhudia shehena hiyo iliyohifadhiwa katika kituo kikuu cha Polisi wilayani Nyamagana baada ya kukamatwa Waziri Jafo aliwapongeza watendaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Uongozi wa Mkoa, Wilaya ya Nyamagana na Kamati Jeshi la Polisi kwa ushirikiano na kufanikisha zoezi hilo.

Waziri Jafo alisema kuwa endapo vifungashio hivyo visingekamatwa vingesambaa mitaani na kutumiwa na walaji na kuendeleza uchafuzi mkubwa wa mazingira hivyo kurudisha nyuma kampeni ya kupiga marufuko mifuko na vifungashio visivyo na viwango.

“Suala Serikali ilishatoa tamko kuwa mwisho wa vifungashio hivi ni tarehe 8 mwezi wa 4 na mimi nilitolea tamko tarehe 8 mwezi huu wa 4 sasa kuna baadhi ya watu wasio na nia njema wanaendelea kusambaza mifuko hii, sasa nina imani watafikishwa haraka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” alisisitiza.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa maelekezo lakini wapo baadhi ya watu wanakaidi hivyo itaendelea kuhakikisha maelekezo yote inayotoa yanafanyiwa kazi na kuwa haitavumilia wanayoyakaidia.


Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Muliro Jumanne alisema ushirikiano wa pamoja kati ya vyombo vya dola na taasisi zingine ikiwemo NEMC ndio umeleta mafanikio hayo.

Aliushukuru uongozi wa wilaya ya Nyamagana pamoja na NEMC kwa kufuatili na jukumu la Jeshi hilo ni kuhakikisha sheria zote zilizotungwa na Bunge ikiwemo zikiwemo zinazohusu masuala ya mazingira zinatekelezwa.

Aliongeza kuwa wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha wanajihusisha na biashara wakubwa kwa wadogo wanaojihusisha na biashara ya mifuko na vifungashio vilivyokatazwa wanakamatwa.

Aliahidi kuendeela kufanya ushirikiano na Ofisi ya Mashtaka ambayo iko kisheria kuhakikisha mwenendo wa kesi unakwenda vizuri na baadaye kupata matokero mazuri.

Meneja wa NEMC wa Kanda ya Ziwa, Redempta Samuel aliwataka wananchi kuacha mara moja kutumia mifuko na vifungashio vilivyopigwa marufu na Serikali kuepuka madhara.

“Sasa ni wakati muafaka wa kuacha kutumia mifuko na vifungashio hivi kwa faida yetu wenyewe kwani inaleta madhara inaziba mifereji, wanyama wanakufa, tukiichoma ule moshi wenye kemikali unatudhuru, hebu tutumie mifuko mbadala kuepuka mgogoro na Serikali,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa kanuni ya 8 ya Katazo la Mifuko ya Plastiki ambayo inataja makosa matano ya kuzalisha, kuingiza, kusambaza, kuuza na kutumia mifuko iliyokatazwa adhabu yake ni faini ya 30,000 hadi sh. bilioni 10 au kifugo hadi miaka miwili.

 

Post a Comment

0 Comments