Apr 20, 2021

Jinsi ya kuepuka utumwa wa mapenzi

  Muungwana Blog 3       Apr 20, 2021
Rafiki zangu, uwanja wa mapenzi ni mpana sana, wakati mwingine unatakiwa kutumia akili na uwezo wako wa mwisho wa kufikiri ili uweze kung’amua ufanyacho kama ni sahihi au lah!

Lakini kama unataka mambo yako yakuendee vizuri zaidi na zaidi na uache kujuta, lazima umshirikishe Mungu. Mweke yeye namba moja katika uhusiano wako, mweke mpenzi wako mikononi mwake na mwisho wa siku utaona mafanikio yake.

Machozi yako hayatamwagika tena ikiwa utamtanguliza yeye. Wengine hujisahau mapema, wanajiona wanaweza kila kitu bila msaada wa Mungu, nani amekudanganya? Usijidanganye ndugu yangu, wengi ambao wanamtumainia Mungu mambo yao huwanyookea.

Katika mapenzi kuna aina nyingi za uhusiano, wengine huwa na mtu kwa muda mfupi wakati wapo ambao wanatamani sana kuishi na wenza wao baada ya kuwa katika uhusiano wa kawaida. Inapendeza sana kama wote mtakuwa mnawaza katika umoja, yaani lililopo kichwani mwako ndilo lililomo kichwani mwa mpenzi wako, vinginevyo lazima mmoja wenu atalia!

Unapokuwa katika uhusiano na mpenzi ambaye moyo wako umemfia na unatamani kufunga naye ndoa, lakini wakati huohuo mpenzi wako huyo hana ‘time’ na jambo hilo ni hatari sana. Inawezekana ukawa unafahamu juu ya jambo hilo na unachojaribu kufanya ni kumlazimisha/ kumshawishi zaidi ili awe na fikra kama zako jambo ambalo mara nyingi husababisha mtafaruku.

Hata hivyo siyo kila aliye katika uhusiano usio na dira ameamua yeye kwa mapenzi yake, wapo wanaolazimishwa na wazazi/walezi lakini pia kuna ambao hudhamiria kuwashawishi wenzi wao wabadili uamuzi ili mwisho wa siku waweze kuolewa.

Kwanza tuangalie maana ya utumwa wa mapenzi kabla ya kupitia vipengele vingine vitakavyokuweka wazi juu ya jinsi unavyoweza kuepukana na uhusiano wa aina hiyo.

Utumwa wa mapenzi
Ni hali ya kuwa/kuishi na mpenzi ambaye humpendi kwa moyo wako lakini unalazimika kuwa naye kwa sababu binafsi. Maana ya pili ni kuwa/kuishi na mpenzi ambaye hakupendi na unajua kabisa hana mapenzi na wewe lakini unalazimisha ukiamini kwamba siku moja anaweza kubadili uamuzi wake.

Aina hizi mbili za utumwa ndizo zinazowasumbua wengi na kuendelea kuteseka katika uhusiano ambao mwisho wake ni matatizo.

Wakati unafanya hayo, unatakiwa ukumbuke jambo moja muhimu; wewe ni mtu mzima na unaendelea kukua, umri unasogea hivyo kuendelea kung’ang’ania penzi la mtu ambaye hana mwelekeo (kwa namna moja kati ya mbili nilizoainisha hapo juu) unajiweka katika nafasi ya kutoingia kwenye ndoa.

Uhusiano bila penzi la kweli
Uhusiano wa aina hii ni ule ambao mmoja wao anakuwa hana mapenzi kwa mwezake lakini analazimisha kuwa naye kwa sababu ya kupata masilahi. Mapenzi ya aina hii siku hizi yameenea sana.

Unakuta mwanamke anaamua kuwa na mwanaume fulani ingawa anajua wazi kwamba hampendi lakini kwa sababu jamaa kashaonyesha mapenzi kwake na anajua wazi anampenda, basi anakubali kwa sababu ya kupata kitu.

Tatizo linakuja pale ambapo jamaa anaamua kufunga naye ndoa moja kwa moja, mara nyingi kwanza huanza kusita lakini baada ya kufikiria kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri kwa marafiki (wenye tamaa kama yeye) huamua kuingia katika ndoa na mwanaume ambaye hajampenda akitegemea kupata maisha mazuri.
logoblog

Thanks for reading Jinsi ya kuepuka utumwa wa mapenzi

Previous
« Prev Post

No comments:

Post a Comment