May 4, 2021

Kenya na Tanzania zatia mikataba ya kibiashara na uwekezaji


Kenya na Tanzania zimetia sahihi mikataba kadhaa ikiwemo ya kibiashara, uwekezaji na mahusiano kwa lengo la kuboresha ushirikiano na urafiki kati ya mataifa hayo ya Afrika Mashariki.

Akizungumza baada ya mazungumzo kati yake na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, Rais Samia Suluhu amesema kuwa atafanya juhudi kuona kuwa Watanzania wanajitahidi kujaza pengo la kibiashara kati ya mataifa hayo.

Rais Samia Suluhu Hassan anazuru Kenya takribani mwezi mmoja na nusu baada ya kuchukua hatamu za uongozi nchini Tanzania. Ziara yake ya pili nje ya Tanzania baada ya kuzuru Uganda majuma matatu yaliyopita, inaonekana kuwa mwamko mpya wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo jirani ya Afrika Mashariki ambayo hayajakuwa na mahusiano mema, chini ya rais John Pombe Magufuli aliyeaga dunia.

Alipowasili mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta alimkaribisha katika Ikulu ya Nairobi alikagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21 kabla ya kufanya mazungumzo. Kenya ni mwekezaji mkuu wa tano nchini Tanzania, ikiwa ya kwanza katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Tanzania tutakuja kwa nguvu zote Kenya ili kuwekeza na ili kukuza ujazo wa biashara,” amesema Rais Samia.

Bishara na uwekezaji kati ya Kenya na Tanzania ni wastan wa dola milioni 450 za Marekani, huku Kenya ikiuza bidhaa nyingi zaidi ya Tanzania. Hata hivyo marais hao wamekubaliana kuondoa vikwazo kwenye mipaka ili kurahisisha biashara kati yazo. Aidha wamewataka matabibu kwenye mipaka kurahisishia wafanyibiashara kuingia na kutoka kwenye mataifa hayo wanapowapima watu ugonjwa wa covid-19.


KWA HABARI ZAIDI <DOWNLOAD HAPA>
Share:
Loading...

Popular Posts

Copyright © MUUNGWANA BLOG | Powered by Blogger