Wakala wa vipimo waanza kutoa elimu ya vipimo, vifungashio kwa wazalishaji na wafanyabiashara wadogo wadogo


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Wakala wa vipimo Tanzania WMA wameanza kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wazalishaji wadogo wadogo namna ya kutumia vipimo sahihi katika ufungashaji wa bidhaa wanazozizalisha ili kukidhi katika masoko ya ndani na kimataifa kwenye bidhaa zao.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa semina hiyo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa vipimo Tanzania WMA Bi. Stellah Kuhwa amesema lengo la semina hiyo ni kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa kuwa na uelewa wa vipimo na viwango sahihi vya bidhaa zao.

Amesema Wakala wa vipimo Tanzania wanajukumu la kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa hapa nchini zinakuwa katika vipimo sahihi na thamani halisi ya bidhaa hiyo ambayo pia inaweza kukidhi viwango vya kimataifa hatimaye kushindana na bidhaa nyingine kimataifa.


“Semina hizi tutafanya nchini nzima na sasa tupo Mkoa wa Dodoma lengo letu ni kuhakikisha wazalishaji wetu wadogo wadogo na wafanyabiashara wanafahamu viwango sahihi vya vipimo ili bidhaa wanazozalisha viwango vyake zikidhi kiwango cha kimataifa tushindane na wengine kimataifa” amesema Bi. Stellah.

Amesema semina hizo zimelenga wazalishaji wa bidhaa za kufungashwa wanakuwa kutoka wazalishaji wadogo kuwa wa kati kisha kuwa wazalishaji wakubwa waende hadi kimataifa kwa kuwa wafanyabiashara wakubwa sana.

Amesema Wakala wanatoa miongozo kwa wazalishaji wa ndani na ambapo wamewataka wafanyabiashara na wazalishaji kufuata miongozo hiyo ili waweze kukidhi matakwa ya kimataifa ambapo Tanzania ni mwanachama na wamelidhia miongozo hiyo katika soko la kimataifa.

Kaimu Meneja wa Wakala wa vipimo Tanzania Mkoa wa Dodoma Karim Zuberi amesema semina hiyo ni mwendelezo wa semina ambazo wamekuwa wakitoa wanapowatembelea wafanyabiashara na wazalishaji mmoja mmoja katika maeneo yao ya kazi ambapo pia wamekuwa wakiwashirikisha watendaji wa kata.

Amesema wamekuwa na utaratibu huo lengo ni kuhakikisha Mkoa wa Dodoma unakuwa bidhaa zilizokidhi viwango vya uzito na kutoa onyo kwa wazalishaji na wafanyabiashara wenye tabia ya kuchezea vipimo kuacha mara moja kwa kuwa sheria ni kali ambapo faini yake huanzia laki moja hadi milioni ishirini kulingana na kosa.

Kwa upande wake Katibu tawala msaidizi Mkoa wa Dodoma sekta ya uchumi Bi. Aziza Mumba aliyekuwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amesema sekta ya vipimo ni nyeti sana kwa uzalishaji wa bidhaa hasa katika kipindi hiki kumekuwa na hamasa kubwa ya uanzishwaji wa viwanda ambapo kwa Mkoa wa Dodoma viwanda zaidi ya elfu tatu vilianzishwa.

Amebainisha kuwa semina hiyo itakuwa chachu kubwa ya uzingativu wa viwango sahihi vya vipimo vya bidhaa katika bidhaa mbalimbali kwani awali walikuwa wakipokea malalamiko mengi kwa wananchi kutokupata vipimo sahaihi vinavyotakiwa katika bidhaa wanazozinunua.

Amesema kuna haja ya mamlaka za serikali za mitaa kutilia mkazo vipimo sahihi katika minada kwani kuna baadhi ya minada hawatumii vipimo sahihi katika bidhaa mbalimbali hasa katika mifugo mara nyingi wamekuwa wakikadiria ukubwa wa mnyama ambapo huwezi kupata thamani halisi ya mifugo.

Nae mmoja wa waliohudhuria semina hiyo Bi. Marry Marnabas ambaye anatoka katika kikundi cha wanawake wapambanaji ambao wanazalisha bidhaa mbalimbali amesema semina hiyo itakuwa msaada mkubwa kwao kwani sasa wamejua viwango sahihi katika vipimo.

“Semina hii ni nzuri naamini tukitoka hapa tutakuwa katika hatua nyingine na tumeona kunahaja ya kutumia vipimo sahihi katika bidhaa zetu ila kuwaibia wateja wetu kutipia vipimo jambo ambalo hata Mungu hapendi” amesema Marry.

 

Post a Comment

0 Comments