https://monetag.com/?ref_id=TTIb DCI Wambura atoa onyo kwa Wahalifu | Muungwana BLOG

DCI Wambura atoa onyo kwa Wahalifu

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Camilius Wambura amesema Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yeyote atakayeendelea  kujihusisha na vitendo vya uhalifu hususani wakati huu ambao Jeshi hilo linaendelea na Operesheni kali ya kupambana na vitendo hivyo.

DCI Wambura ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowashirikisha Maofisa wa Makao Makuu ya Upelelezi na Wakuu wa Upelelezi wa mikoa nchini kwa lengo la kupanga mikakati ya kupambana na uhalifu  pamoja na kutathmini hali ya uhalifu nchini.


Alisema mtu yeyote amabaye anajihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja kwakuwa mkono wa Jeshi la Polisi ni mkubwa  na kwa wakati huu hakuna upenyo wowote utakaoachwa kwa kuwa Operesheni inaendelea nchi nzima.

Alisema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ameona ni bora kukutana na Wakuu hao wa Upelelezi kutoka Mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar ili kwa pamoja waweke mikakati ya pamoja ambayo italenga kutokomeza uhalifu hapa nchini.

“ Wito wangu kwa wahalifu ni bora   watafute kazi nyingine ya kufanya kwa kuwa hatuna huruma kwa watu hao na Wananchi waendelee kutupatia taarifa zao ili tuhakikishe nchi yetu inaendelea kuwa salama “ Alisema Wambura.

Kwa upande wake Naibu DCI, DCP Faustine Shilogile alisema Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Makao Makuu inaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu na utoaji wa mafunzo kwa watendaji wa idara hiyo ili kuwa na wapelelezi wenye weledi ambao watasaidia kuharakisha upelelezi wa kesi zinazoripotiwa katika vituo vya Polisi.

Katika kikao hicho Wakuu wa Vitengo kutoka  Idara ya Upelelezi wa Makao Makuu ya Polisi walipata fursa ya kutoa elimu kwa Wakuu hao wa Upelelezi wa mikoa jinsi Vitengo vyao vinavyofanya kazi pamoja na Mwakilishi wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka.

 

Post a Comment

0 Comments