Kenya kukopa shilingi bilioni 2.6 kufadhili oparesheni zake



Serikali ya Kenya inalazimika kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2.6 kufadhili operesheni zake kama inavyoelezwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/22.

Bajeti hii ya shilingi trilioni 3.66 ndiyo ya mwisho ya mwaka mzima kamili wa fedha ambayo serikali ya Jubilee itamiliki kabla ya muhula wa uongozi kukamilika mwakani.Vita dhidi ya corona vimepata msukumo mpya baada ya wizara ya elimu kutenga fedha za ziada kununua chanjo.

Hii ni bajeti ya pili kusomwa tangu janga la corona kuutikisa ulimwengu. Muda mfupi baada ya saa tisa alasiri, Spika wa bunge la taifa alimkaribisha Waziri wa fedha wa Kenya Ukur Yattani kupanda jukwaani

"Ripoti ya kamati ya bunge ya bajeti imekamilika. Kama sehemu ya mchakato, waziri wa fedha analazimika kuweka bayana makadirio ya bajeti ya mwaka 2021/2022. Ni furaha yangu kumualika waziri wa fedha Ukur Yattani kuitangaza rasmi bajeti ya mwaka mpya wa fedha 2021/2022 kabla ya saa tisa kupita."

Kikubwa kilichojitokeza katika bajeti mpya ya mwaka 2021/22 ni nakisi ya shilingi bilioni 952 kukimu mahitaji ya operesheni za mwaka mpya wa fedha. Kwenye hotuba yake, waziri wa Fedha wa Kenya, Ukur Yattani ameongeza kiwango cha fedha zilizotengewa sekta zinazoaminika kuwa mstari wa mbele kuisukuma ajenda ya nguzo nne za maendeleo na uchumi. Wizara tano zilizotengewa fedha nyingi zaidi ni za Fedha, Ulinzi,Afya, Maji/Kilimo na Nishati ambazo ni shilingi trilioni 1.63.Serikali za kaunti zimetengewa shilingi bilioni 370 kufadhili operesheni mikoani.

"Nia yetu ni kuendelea kupunguza idadi ya wanaopata punguzo la kodi ili kuleta usawa na kuliongeza pato kufadhili miradi ya kijamii ili kupunguza nakisi. Kwenye bajeti hii nitapandekeza hatua kadhaa za kuliongeza pato la jumla. Rasimu ya sera ya kodi ya kitaifa iko tayari na wadau watasambaziwa kabla ya umma kutoa mchango wao na bunge kuipa ridhaa."

Bajeti mpya imeongezeka kutokea shilingi trilioni 2.8 hadi 3.6.Hata hivyo serikali imepunguza gharama za matumizi kwa shilingi bilioni 8.7.Sekta za Elimu,Idara ya usimamizi wa jiji la Nairobi na Viunga vyake pamoja na kampuni ya kuzalisha umeme zimepunguziwa fedha za kugharamia operesheni zao japo walimu wa ziada wataajiriwa.

Itakumbukwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta aliposhika hatamu za uongozi aliweka bayana kuwa azma yake ni kuisukuma ajenda ya nguzo nne kuu za maendeleo. Sekta za viwanda vya nguo na uzalishaji zimepewa nguvu mpya ili kuunda nafasi za ajira kwa vijana. Mpango wa kazi mitaani unaowalenga vijana umeongezewa shilingi bilioni 3 ili kuwapiga jeki waliopoteza ajira kwasababu ya janga la corona.Ili kuimarisha mapambano ya COVID 19, wizara ya afya imetengewa shilingi bilioni 14.3 kugharamia chanjo.

Kinachowatia wasiwasi wakenya ni kuwa kwa kila shilingi 100 ambayo mamlaka ya kukusanya kodi,KRA, itachukua zaidi ya nusu zitatumika kulipia madeni. Haya yanajiri wakati ambapo janga la corona limeuvuruga uchumi na wakenya kupoteza ajira kwa mwaka wa pili mfululizo.

Amos Kimunya, ambaye ni kiongozi wa chama tawala bungeni amesema, "Hii bajeti inamsaidia mwananchi wa kawaida kwani kuna pesa zilizotengewa sekta ya afya ukizingatia janga la Covid-19. Kuna pesa zimetengwa kufadhili biashara ndogo ndogo na miradi iliyoanzishwa na haijakamilika. Pia madeni yote lazima yalipwe katika taasisi za serikali. Kwa hiyo haijakuwa na ongezeko la kodi kwa wananchi."

Serikali inajiandaa kuzindua ifikapo Julai mwaka 2022 mpango maalum wa malipo ya uzeeni unaowalenga waliojiari maarufu sekta ya Jua kali.Bidhaa za ujenzi za chuma zitaruhiswa kuagizwa kutoka nje kwa kodi ya 25% ili kuwalinda watengezaji wa humu nchini.Takwimu za Benki Kuu ya Kenya zinaonyesha kuwa deni la taifa limefikia shilingi trilioni 7.339.Taasisi za serikali zimetakiwa kulipa madeni ya operesheni ifikapo mwisho wa mwezi wa Juni.

Post a Comment

0 Comments