Kilwa yapata Hati safi miaka mitano mfululizo

 


Kwa miaka mitano ya fedha kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 Wilaya ya Kilwa imekuwa ikipata hati inayoridhisha katika ukaguzi unaofanywa na ofisi ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG). Katika kipindi hicho taarifa za ukaguzi kwa mujibu wa taratibu za ukaguzi umeonesha kuwa utunzaji wa kumbukukumbu wa taarifa , ukusanyaji wa mapato na matumizi umekidhi sifa za kikaguzi.

Taarifa hiyo ya ukaguzi wa taarifa za mwaka wa fedha 2019/2020 kama ilivyowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa nje wa Mkoa wa Lindi ndugu Deogratius Patrick Mtenga  ambaye aliwasilisha taarifa yake katika baraza maalum la Madiwani ambayo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe.Zainab Telack pamoja na Katibu tawala wa Mkoa wa Lindi Bi.Rehema Madenge.

Katika taarifa hiyo, ndugu Mtenga alianza kwa kutoa ufafanuzi wa maana halisi ya hati ya ukaguzi ambapo alieleza kuwa ‘’Hati ya ukaguzi ni maoni huru ya Mkaguzi inayoeleza kama taarifa za fedha zilizokaguliwa zimetayarishwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu za mwisho na miongozo inayotolewa na Hazina kwa kushirikiana na bodi ya Uhasibu kwa mujibu wa misingi inayotumika katika uandaaji wa taarifa hizo’’.

Mkaguzi huyo pia alizitaja aina ya hati zinazotolewa baada ya ukaguzi kuwa ni ; Hati inayoridhisha , Hati yenye Mashaka, Hati isiyoridhisha pamoja na Hati mbaya.

Katika ukaguzi huo wa mwaka wa fedha 2019/2020 Jumla ya hoja sitini na moja (61) zilikaguliwa na hoja zote sitini na moja zilijibiwa ambapo pamoja na hoja zote kupatiwa majibu lakini hoja zilizofungwa ni thelathini na mbili(32) huku hoja ishirini na tisa(29) zikiwa bado hazijafungwa na hivyo kuitaka Baraza la madiwani kuendelea kuzitafutia majibu ili nazo ziweze kufungwa. 

Mkaguzi huyo Mkuu wa nje wa Mkoa wa Lindi ndugu Deogratius Patrick Mtenga alizitaja baadhi ya hoja zilizokaguliwa kuwa ni pamoja na Halmashauri kuchelewa kuuza mali chakavu, kutoteketezwa kwa madawa yaliyoisha muda wake, baadhi ya Magari ya Halmashauri kuwa na namba binafsi pamoja na Watumishi kukaimu kwa muda mrefu katika nafasi za ukuu wa Idara na Vitengo.


Akiwasilisha majibu ya kamati ya fedha kwenye baraza hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndugu Renatus Mchau alisema hatua mbali mbali zimeshachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuindikia Wizara ya Fedha na Mipango  kuomba Kibali cha uteketezaji na kuwa tayari kibali cha utekezaji kimeshapatikana mwaka huu tarehe 15/6/2021, na katika hoja ya Watumishi kukaimu muda mrefu Mkurugenzi huyo alisema baadhi ya watumishi hao walikosa sifa za nafasi wanazozikaimu na hivyo utaratibu unafanyika wa ama kuwaombea vibali vya kuendelea kukaimu au kujaza nafasi endapo watu wenye sifa zinazohitajika watapatikana.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe.Zainab Telack ambaye ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika Wilayani Kilwa tangu alipoteliwa kushika nafasi hiyo , aliwapongeza kwa kupata hati hiyo huku akiwataka kuchukua hatua za haraka katika hoja ziliobaki ili ziweze kufungwa. ‘Nimesikia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za serikali, nawapongeza sana lakini niwatake hizo hoja zilizobaki zinafanyiwa kazi ili nazo ziweze kufungwa’’.

Mhe.Telack alitumia nafasi hiyo kuwataka waheshimiwa madiwani kufanya kazi kwa pamoja na wataalam ili kuweza kutatua changamoto kwa haraka. ‘’Waheshimiwa Madiwani , nyie ndiyo wasimamizi wa halmashauri kwa mujibu wa sheria ,lakini usimamizi wenu utafanikiwa tu endapo mtafanya kazi kwa kushirikiana, kukiwa na mvutano kati yenu nyote mtakwama na  mkikwama mtakuwa mmemkwamisha Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Tanzania ambaye anaamini nyie kwa nafasi zenu mna uwezo wa kuwaletea wananchi wenu maendeleo’’ alihitimisha Mhe.Telack.


Akifunga baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Farida Mohamed Kikoleka aliwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku akimhakikishi Mhe.Mkuu wa Mkoa kuwa Halmashauri anayoiongoza ina ushirikiano mkubwa sana na watumishi na hivyo asiwe na wasiwasi Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Post a Comment

0 Comments