Prof. Ndalichako kufungua mashindano ya UMISSETA kesho uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Joyce Ndalichako kesho Juni 21, 2021 anatarajia  kufungua Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) kwenye Uwanja wa  Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.  

Mashindano haya yanajumuisha mikoa yote kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambapo yatafanyika kwenye  viwanja vya Nangwanda Sijaona, Chuo cha Walimu Mtwara (TTC kawaida) Chuo cha Walimu Ufundi maarufu  kama Mwasandube, na viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara ambapo yanaanza kesho Juni 21, 2021 na kumalizika Julai 03, 2021. Mashindano yameandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Michezo na TAMISEMI chini ya Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo. 

Mashindano haya yalitanguliwa na Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Kassim Majaliwa Majaliwa Juni 8, mwaka huu mjini Mtwara na kufungwa na Naibu Waziri wa Habari,  Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul Juni 18, 2021. 

Michezo itakayoshindaniwa katika mashindano haya ni mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira  wa miguu maalum kwa wavulana (wenye ulemavu wa kusikia) mpira wa pete, mpira wa wavu kwa wasichana  na wavulana, mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana, mpira wa kikapu kwa wasichana na wavulana, mpira wa meza kwa wasichana na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma. 

Aidha, kutakuwa na mashindano ya usafi katika mazingira wanayoishi. Mashindano yatapambwa na wasanii  mbalimbali wa kizazi kipya wakiongozwa na Mauwa Sama na Chege ili kutoa hamasa na burudani. Pia vyama  vya michezo, mashirikisho na vilabu vya michezo mbalimbali vimealikwa kuja kuangalia vipaji mbalimbali. 

Kauli mbiu ya michezo ya mwaka huu ni “Michezo, Sanaa na Taaluma kwa Maendeleo ya Uchumi wa  Viwanda” 

 

Post a Comment

0 Comments