Wabunge wa Mtwara wapambania umeme

 


Wabunge wa Mkoa wa Mtwara wameungana ili kuhakikisha kuwa mradi kabambe wa kusambaza umeme unawafikia wananchi wote mitaani na vijijini hususani Jimbo la Tandahimba lenye idadi kubwa ya vijiji visivyo na umeme.


Akizungumza mbele ya Waziri wa  Nishati Dk Medard Kalemani katika uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili Mbunge Tandahimba Katani Ahmad Katani amesema ujio wa umeme huo utaongeza hamasa ya maendeleo nchini.


Amesema kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika kwa kukosa umeme kwa muda mrefu ni jimbo la Tandahimba ambalo lina vijiji 143 huku vijiji 54 vina na umeme na 89 havina.


"Uzinduzi huu tunaimani utaleta tiba ya kuwa na umeme wa uhakika kwenye vijiji vyote ambavyo awali havikuwa na huduma hiyo ikiwemo vijiji 89 vya Wilaya ya Tandahimba" alisema Katani


Naye Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cecil Mwambe amesema kuwa umeme uliopo katika jimbo hilo hautoshelezi hivyo ujio wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili utasaidia na kutatua changamoto hiyo


"Katika Jimbo la Ndanda hatuna tatizo la kukosa umeme kabisa japo zipo kata za Mpanyani na Msikisi  hazina umeme kabisa ndio maana tumeomba zianzwe hizo ili kupunguza tatizo hilo sisi tuna Vijiji 66 lakini 30 havina umeme tunajua Serikali itaweka kila Kijiji huduma hii kazi hii itatekelezwa kwa ubora wake" amesema Mwambe


Naye Mbunge wa Jimbo la Lulindi Rajabu Mchungahela,  amesema kuwa sasa wana uhakika kuwa huduma ya umeme itapatikana katika mkoa mzima wa Mtwara na katika vijiji vilivyotajwa kukosa huduma ya umeme.


Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini  Hassan Mtenga amesema ujio wa awamu hiyo ya usambaji wa umeme itasaidia wananchi ingawa Mtwara bado tatizo la umeme ni kubwa.


"Mtwara Mjini bado kuna shida ya umeme japo tunaona wanavyopambana lakini bado hali si nzuri, tunafahamiana kuwa haikuwa kazi nyepesi kwa Waziri huyu kufika hapa na kufanya uzinduzi huu" alisema Mtenga


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo  la Nanyamba Abdallah Chikota amesema kuwa wanafurahi kusikia Serikali ikisema kuna  vijiji zaidi 400 vitaunganishiwa umeme.


 "Kwa jitihada hizi ifikapo 2022 halmashauri yetu yote itakuwa na umeme na hii kazi itaanzia katika Kijiji cha Namtumbuka tunahitaji umeme ili itusaidie kutatua changamoto ya ulinzi katika maeneo yetu”, amesema Chikota

Post a Comment

0 Comments