Ufaransa yashutumu uchokozi wa Erdogan kuhusu Cyprus


 Ufaransa imemshutumu Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kwa uchokozi, baada ya kushinikiza suluhisho la mataifa mawili katika suala la Cyprus. 


Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, wakati wa ziara yake kwenye eneo linalokaliwa na Uturuki kaskazini mwa kisiwa hicho cha Mediterrania. Le Drian amesema Ufaransa inasikitishwa na hatua ya upande mmoja iliyochukuliwa na Uturuki ambayo haikuratibiwa na inasababisha uchokozi. 


Maafisa wa Cyprus ya Uturuki walichukua hatua ya peke yao ya kufungua tena mji uliotelekezwa wa Varosha kwa lengo la kuanzisha makaazi. Le Drian amesema alilijadili suala hilo Julai 20 na waziri mwenzake wa Cyprus na ataliwasilisha katika Umoja wa Mataifa.


Mji wa Varosha uliachwa tangu mwaka 1974 wakati vita vilipokigawa kisiwa hicho. Cyprus ya upande wa Ugiriki ina wasiwasi kwamba Uturuki inakusudia kuuchukua mji huo. Rais wa Cyprus, Nicos Anastasiades ameielezea hatua hiyo kama isiyo halali na isiyokubalika.

Post a Comment

0 Comments