Mawaziri watembelea kiwanda cha kuchakata mpunga


Waziri wa kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha uzalishaji katika zao la mpunga unaongeza kutoka tani mbili zinazozalishwa kwa sasa hadi kufikia tani nne kwa hekta moja.


Prof. Mkenda aneyasema hayo leo mjini Morogoro akiwa kwenye ziara ya pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo baada ya kutembelea kiwanda cha kuchakata mpunga cha MW Rise ambacho kimekuwa kikinunua mpunga kutoka kwa wakulima na kuukoboa, kuweka madaraja, kufungasha kisha kuuza ndani na nje ya nchi.


Alisema kuwa kwa sasa wakulima kwa ujumla wanauwezo wa kuzalisha tani milioni tatu za mchele huku matumizi ya nchi yakiwa ni tani 1.3 milioni na hivyo kumekuwa na ziada ya mchele.


Kufuatia ziada hiyo Waziri Mkenda alisema kuwa ni lazima kama ubora wa mchele unaozalisha hapa nchini uongezeke ili kuweza kupata masoko ndani na nje ya nchi na kwamba njia nzuri ya kuongeza ubora ni kuwa na viwanda vya kuchakata mpunga na kuweka katika hali ya usafi na inayovutia.


Alisema kuwa lengo la ziara hiyo yeye na waziri mwenzake waweze kuona namna kiwanda hicho kinavyozalisha na kusikiliza changamoto zilizopo kwenye uzalishaji ili Serikali iangalie namna bora ya kuweza kutatua.


Aidha Waziri Mkenda alisisiza wakulima kuongeza uzalishaji ambapo alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya ‘Wilmar’wamekubaliana kuanzisha vituo vya mashamba darasa kwa ajili ya wakulima ambao watapatiwa huduma ya ugani.


“Sasa hivi kwa wastani hekta moja tunaweza kupata tani mbili za mpunga, lakini wenzetu kama Thailand wanapata tani nane za mpunga na hiyo ni kutokana na wao wenzetu kutumia zaidi kilimo cha umwagiliaji, sasa sisi lengo letu tuongeze uzalishaji kutoka tani mbili hadi kufikia tano tatu hadi tano za mpunga ili kwenye soko la nje tuweze kupata ushindani,” alisema Mkenda.


Alisema kuwa tayari wizara hiyo imeshapeleka andiko Tamisemi kwa ajili ya kuainisha maeneo ambayo yanayofaa kuanzisha mashamba darasa hayo na pia tayari wizara imeshaainisha maeneo yatakayotumika kama vituo vya kukusanya, kuhifadhi na kukausha mpunga kabla ya kufikishwa kiwandani.


Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitala Mkumbo alisema kuwa katika kutekeleza irani ya CCM wizara imeweka msisitizo zaidi kwenye viwanda vya kuongeza thamani hasa kwenye bidhaa za kilimo.


Prof. Mkumbo alisema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kisera, kisheria na miongozo ili wawekezaji wenye viwanda na wafanyabiashara waweze kufanya shughuli zao na kuongeza uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja.


Awali akitoa taarifa Meneja rasilimali watu wa kiwanda hicho Deusidedit Kikuna aliishukuru Serikali kupitia wizara ya Kilimo na wizara ya Viwanda na Biashara kwa kupata ushirikiano katika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa kiwanda hicho.


Akizungumzia uzalishaji wa kanda hicho Kikuna alisema kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha tani 288 za mchele kwa siku na kwamba kama Serikali itaweza kutatua baadhi ya changamoto uzalishaji huo utaongezeka zaidi ya mara tatu kuliko ilivyo sasa.

Post a Comment

0 Comments