Naibu Waziri Ulega ahimiza wafugaji kulima malisho ya mifugo

 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wafugaji hapa nchini kulima malisho kwa ajili ya mifugo yao.


Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo wakati alipotembelea shamba la malisho ya mifugo kwenye kitalu cha NARCO ambacho kinatumiwa na Kampuni ya Kahama Fresh wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.


Akiwa katika shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 400, Naibu Waziri Ulega amesema wafugaji wanatakiwa kulima malisho na kuacha kutegemea malisho ya asili peke yake. Lakini pia amesema ipo fursa kubwa kupitia kilimo cha malisho kwa wafugaji na wasio wafugaji kwani kufanya biashara ya malisho ya mifugo kutawawezesha kujinyanyua kiuchumi.


Naibu Waziri Ulega ametembelea kuona ujenzi unaoendelea wa kiwanda cha vyakula vya mifugo pamoja na kiwanda cha maziwa, ambapo ameipongeza Kampuni ya Kahama Fresh kwa kuamua kufanya uwekezaji huo. Vilevile ametembelea kuona mifugo inayomilikiwa na Kampuni hiyo ambapo amesema kuwa mwekezaji huyo ameonesha mfano mzuri wa matumizi ya ardhi aliyokodoshiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kuwataka wawekezaji wengine kufuata taratibu wanazopewa.


Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Ntangeki amesema kwa upande wa kiwanda wanatarajia kiwe kimekamilika ifikapo mwezi Machi, 2021. Lakini kwa sasa wanaendeleo kutoa mitamba kwa ajili ya maziwa kwa wafugaji wadogo ambao ndio watakuwa wakipeleka maziwa kwenye kiwanda hicho kitakapo kamilika.

Post a Comment

0 Comments