Ticker

6/recent/ticker-posts

Nape amshukia Polepole akihoji orodha ya wahuni

 


Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amemtaka Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole kuwataja watu aliowaita kuwa ni wahuni aliosema hawakushughulikiwa wakati wa utawala wa Awamu ya Tano.


Kauli ya Nape imekuja kufuatia mahojiano aliyofanya Polepole na kituo cha televisheni cha Wasafi ambapo pamoja na mambo mengine, alisema udhaifu wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kushindwa kuwamaliza wahuni.


Akitoa maoni katika ukurasa wake wa Twitter, Nape alihoji kama kulikuwa na orodha ya wahuni wanaoshughulikiwa.


“Duh! Kumbe kulikuwa na orodha!!Man gesturing (mtu anaashiria) ok, Natamani kujua wahuni waliopona! Rolling on the floor laughing (nabiringika sakafuni nikicheka).


Hata alipoulizwa kwa simu na Mwananchi leo Jumamosi Novemba 27, 2021 Nape alikiri kuandika ujumbe huo akisema, “Mimi nadhani mchukue tu hiyo tweet. Nimeuliza, kumbe kulikuwa na orodha na hao waliobaki ni kina nani?”


Polepole aliteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Desemba 2016 akimrithi Nape aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.


Katika mahojiano hayo yaliyosambaa katika mitandao ya jamii, Polepole aliulizwa kama kuna udhaifu uliokuwepo katika utawala wa Awamu ya Tano.


“Mimi nilikuwa nimetamani sana tuwe tumeshughulika na wahuni wengi tumewamaliza, lakini nafikiri Rais Magufuli na Mama Samia hawakufanikiwa kushughulika na wahuni, kwa hiyo tumebaki nao, kwa hiyo ukiniuliza jambo gani la udhahifu, nakwambia bwana hatukufanikiwa kummaliza wahuni.


“Wahuni bwana, wanakwepa kodi, wahuni wanaonea wanyonge, wahuni wanasema wewe unanijua mimi? Ilikuwa ndoto yangu kushughulika na wahuni ulalo ulalo, angalau wabaki hata asilimia 10, lakini hiyo kazi sidhani kama Rais Magufuli aliimaliza,” alisema Polepole katika mahojiano hayo.


Polepole alipoulizwa kuhusu kauli ya Nape, alimtaka mwandishi kurejea mahojiano hayo.


“Kauli yangu ya leo, sitataka kusema lolote, ila chochote kuhusu kauli zangu kirejewe kwenye mahojiano niliyofanya na Wasafi,” amesema Polepole.


Mbali na suala hilo, Polepole aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM tangu mwaka 2017 hadi 2021, alizungumzia suala la ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo alihoji kutokuwepo kwa mkataba wa bandari hiyo iliyozinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.


Mengine aliyozungumzia ni suala la Katiba mpya, madai ya kununua wapinzani na sakata la wamachinga kuhamishwa kwenye maeneo yao.

Post a Comment

0 Comments