Njia 10 za kuepuka madeni

 

Hakuna mtu anayependa kuwa na madeni, lakini mara nyingi watu hujikuta katika madeni makubwa. Kwa kiasi kikubwa watu wengi huingia kwenye madeni kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha matumizi kuliko kipato.

Madeni siyo kitu kizuri hasa ikiwa hayatalipwa kwa wakati. Swala la kuepuka madeni ni swala linalohitaji maamuzi sahihi ya kifikra pamoja na mikakati stahiki.

Je unapenda kuepuka au kupunguza kiwango chako cha madeni? Karibu nikufahamishe njia 10 za kuepuka madeni.

1. Jiwekee bajeti binafsi
Utawasikia watu wakikosoa bajeti ya serekali lakini hawana bajeti zao binafsi. Bajeti binafsi ni muhimu kwani hukuwezesha kupanga juu ya mapato na matumizi yako.

Ili kuepuka madeni, ni muhimu kuweka bajeti binafsi ambayo itakuongoza juu ya matumizi yako ya pesa ili usije ukatumia kuliko kipato chako.

2. Epuka matumizi yasiyo ya lazima
Kuna matumizi chungu nzima ya pesa, lakini matumizi ya lazima ni machache. Ikiwa kipato chako ni kidogo hakuna haja ya kufanya mambo kama vile kununua simu au nguo za gharama kubwa.

Nimeshuhudia baadhi ya watu wakikopa mikopo kwa ajili ya sherehe na matumizi mengine ya anasa. Mambo kama haya huwaingiza watu wengi kwenye madeni makubwa, hivyo yakupasa kuyaepuka.

3. Epuka kukopa bila mpango
Watu wengi hushindwa kurejesha mikopo kutokana na kukopa bila mpango. Inatakiwa kabla ya kukopa uhakikishe una mpango mzuri unaoonyesha jinsi utakavyotumia na kurejesha mkopo huo.

Kumbuka pesa ya mkopo hasa kutoka kwenye taasisi za kifedha inatakiwa irejeshwe kwa wakati tena kwa riba. Hivyo epuka kutumia pesa za mkopo bila mpango unaoeleweka vyema.

4. Epuka ushawishi wa marafiki kwenye matumizi
Watu wengi hutumbukia kwenye matumizi makubwa au yasiyo na ulazima kutokana na ushawishi wa marafiki kwenye matumizi yao ya pesa.

Hakikisha kila unachokinunua au kutumia pesa yako kina maana kwako na hakitakupotezea pesa zako. Kumbuka mrejeshaji wa mkopo ni wewe na wala siyo rafiki yako.

5. Tumia vizuri huduma
Kutumia vizuri huduma kama vile maji, simu, umeme, gesi au hata mafuta kutakuwezesha kuokoa kiasi kikubwa cha pesa. Kwa mfano hakuna haja ya kukopa kifurushi cha simu, ili tu kuchati au kumsalimia rafiki yako.

Hakikisha kila pesa unayoweka kwenye huduma haipotei. Hili litakuokolea pesa nyingi ambazo utazitumia kwa mahitaji mengine na kuepuka madeni.

6. Tumia kidogo kuliko unachopata
Mara nyingi matumizi huwa makubwa kuliko kipato; na hii ndiyo sababu kubwa ya watu kukopa pesa. Hakikisha unajitahidi kutumia pesa kidogo kuliko zile unazozipata ili ujiwekee akiba na uweze kukidhi mahitaji yako ya msingi.

7. Weka akiba
Kuna kipindi cha shibe na njaa kwenye uchumi; hivyo unahitaji kujiandaa kwa vipindi vyote. Mara nyingi watu hukopa pindi wawapo na uhitaji.

Kwa njia ya kujiwekea akiba utaweza kuwa na pesa hata wakati huna kipato. Kumbuka! Kuweka akiba siyo kuwa na pesa nyingi bali ni maamuzi tu.

8. Lipa madeni kwa wakati
“Dawa ya deni ni kulipa.”

Kwa hakika dawa ya deni ni kulipa, tena kwa wakati na si kulimbikiza. Kutolipa deni kwa wakati hukufanya ujiwekee mzigo mkubwa mbeleni na wala si kupunguza chochote.

Inakupasa kulipa madeni kwa wakati, hasa madeni ya taasisi za kifedha kwani kutolipa kwa wakati kutakufanya uongeze riba ya mkopo zaidi.

9. Jiondoe kwenye huduma zisizokuwa za lazima
Je umejiunga kwenye huduma kama vile bima au vifurushi vya televisheni visivyokuwa vya ulazima? Hakikisha huduma zote zinazokugharimu pesa ambazo si za lazima unaziepuka.

Kwa njia hii utaweza kupunguza matumizi yako na kuokoa pesa kwa ajili ya matumizi mengine, jambo hili litakuwezesha kuepuka kukopa.

10. Tafuta chanzo kingine cha kipato
Mara nyingi milango ya kutoa pesa ni mingi kuliko ile inayoleta pesa. Ni muhimu kutokutegemea chanzo kimoja cha pesa kwani kikikwama au kuzidiwa itakubidi ukope.

Hakikisha unabuni chanzo kingine cha pesa hata kama ni kidogo. Kumbuka “kidogo kidogo hujaza kibaba”.

Neno la mwisho

Kwa hakika nidhamu ya matumizi ya pesa ni jambo muhimu sana katika kuepuka madeni. Naamini pia kama utazingatia hoja jadiliwa hapo juu huku ukihakikisha unakuwa na matumizi mazuri ya pesa, utaweza kupunguza kama siyo kuepuka madeni maishani mwako.

Post a Comment

0 Comments