Mwandishi Salman Rushdie apumulia mashine baada ya kuchomwa visu New York


Mwandishi wa habari aliyezaliwa India, Salman Rushdie, anapumulia mashine hospitalini baada ya hapo jana kushambuliwa akijitayarisha kutoa mhadhara jijini New York, Marekani. Mashahidi wanasema mshambuliaji alipanda kwenye jukwaa ghafla na kumchoma visu mara kadhaa mwandishi huyo wa kitabu cha Aya za Shetani. 


Wakala wake, Andrew Wylie, anasema Rushdie amejeruhiwa ini, mishipa ya damu na huenda akapoteza jicho moja. Polisi inamshikilia mshambuliaji iliyemtaja kwa jina la Hadi Matar, mwenye umri wa miaka 24. 


Rushdie, mwenye umri wa miaka 75, ameishi miaka mingi akiwa chini ya ulinzi wa polisi, kutokana na fatwa ya kifo dhidi yake iliyotolewa mwaka 1989 na kiongozi mkuu wa wakati huo wa Iran, Ayatullah Khomeini, baada ya mwandishi huyo kuandika riwaya yake ya nne, Aya za Shetani, ambayo inatajwa kuukashifu Uislamu. 


Ingawa baadaye Iran ilijitenga na fatwa hiyo, lakini mwaka 2015, Wakfu wa 15 Khordad wa nchi hiyo ulitangaza zawadi ya dola milioni 3.3 kwa yeyote atakayemuuwa Rushdie.

Post a Comment

0 Comments