Wawili Babati Jela kwa kukutwa na meno ya Tembo.


Na John Walter-Babati 

Mahakama ya wilaya ya Babati mkoani Manyara imewakukumu kwenda jela miaka 24 Fred Meibuko (28) mkazi wa mvugue mkoani Tanga na Issa mafita (30) mkazi wa gedamara kata ya gallapo wilayani Babati kwa kosa la kukutwa na jino moja la tembo ambalo ni nyara ya serikali kinyume cha sheria.

Akisoma shauri hilo la jinai mbele ya mahakama hiyo hakimu  wa wilaya ya Babati Victor Kimario amesema watuhumiwa hao walikutwa na kosa hilo la kukutwa na nyara hiyo ya serikali yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 49 tarehe 4 novemba mwaka jana 2023 majira ya saa 6 mchana katika eneo la gallapo wakiwa wanasafirisha kuelekea Babati kwa kutumia usafiri wa pikipiki.

kwa upande wake wakili wa serikali Leonce Bizimana ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ambayo itakuwa  ni fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo  kwakua mnyama tembo anahusika katika utalii na analiingizia taifa fedha za kigeni kutoka kwa watalii.

Naye wakili wa utetezi Abdalla Kilobwa ameiomba mahakama kuwapunguzia kifungo washtakiwa hao ambao bado ni vijana na wananguvu za kufanya kazi kwa kuwa ndio kosa lao la kwanza kushtakiwa.

Aidha akitoa hukumu hiyo hakimu Kimario amesema kwa kuzingatia utetezi wa upande wa washtakiwa hao na upande wa utetezi wa serikali mahakama hiyo  imejiridhisha pasi na shaka na imewakukumu kwenda jela miaka 24 kila mmoja na kuamuru jino hilo la tembo kukabidhiwa kwa mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori kwaajili ya kutunza ushahidi na kuliweka katika kumbukumbu za serikali.

Post a Comment

0 Comments