Na John Walter Hanang’
Mradi mkubwa wa ujenzi wa stendi ya kisasa katika mji wa Katesh, Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, umefikia hatua ya mwisho ya utekelezaji, na unatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Mradi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 5 umetajwa kuwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika mkoa wa Manyara kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kuinua uchumi wa wananchi.
Kwa umuhimu mkubwa wa stendi hiyo ambayo itakuwa mfano kwa mkoa mzima wa Manyara imepewa jina la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, amesema ujenzi huo umefikia asilimia 95 na maandalizi ya mwisho yanaendelea ili kuhakikisha huduma zinaanza kutolewa kama ilivyopangwa.
“Mradi huu ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri na biashara ambapo kukamilika kwake kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hili,” alisema Sendiga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, amepongeza utekelezaji wa mradi huo akisema ni uthibitisho wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo.
“Nimefurahishwa sana kuona mradi huu mkubwa unaelekea kukamilika, hiuu ni ushahidi kuwa serikali ya CCM inatekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi,” alisema Toima.
Stendi hiyo ya kisasa inatarajiwa kutoa huduma kwa magari ya abiria ya ndani na nje ya mkoa, na itakuwa na maeneo ya biashara, ofisi, pamoja na huduma mbalimbali kwa abiria, hatua itakayosaidia kuinua uchumi wa wakazi wa Katesh na maeneo jirani.
0 Comments