F Fountain Gate FC yawaita Wananchi Tanzanite Kwaraa | Muungwana BLOG

Fountain Gate FC yawaita Wananchi Tanzanite Kwaraa



Na John Walter -Babati 
‎Baada ya kupata ushindi muhimu wa mabao 3–1 dhidi ya Stand United katika mchezo wa awali wa play off uliochezwa ugenini, klabu ya Fountain Gate imewaalika mashabiki na wakazi wa Babati kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo wa marudiano utakaopigwa Julai 8, 2025 kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
‎Kocha wa Fountain Gate, Mohammed Laizer, amesema ushindi walioupata kwenye mchezo wa kwanza umetokana na mbinu walizopanga baada ya kubaini udhaifu wa wapinzani wao Stand United, na kwamba mbinu hizo wataziboresha zaidi ili kuhakikisha ushindi wa nyumbani na kufanikiwa kusalia kwenye Ligi Kuu.
‎Kwa upande mwingine, Kocha wa Stand United, Juma Masoud, amesema pamoja na kupoteza mchezo wa kwanza, bado wana matumaini ya kupanda Ligi Kuu endapo watapata ushindi kwenye mchezo wa marudiano. 
‎Ameeleza kuwa matokeo ya awali yamewaumiza, lakini watajitahidi kupindua matokeo kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa Julai 8.
‎Mkurugenzi wa Mashabiki wa Fountain Gate FC, Nickson Sawe, amewaomba wakazi wote wa Babati kufika kwa wingi kushuhudia mechi hiyo ya mwisho ya msimu dhidi ya Stand United kutoka Shinyanga. 
‎Amesema uwanja wa Tanzanite Kwaraa ni kama “jehanamu kwa mpinzani” na hakuna atakayeshinda kwa urahisi.
‎Naye msemaji wa Fountain Gate, Issa Mbuzi, amewahakikishia mashabiki na wakazi wa Babati kuwa furaha waliyoikosa msimu huu itarejea kwa nguvu kubwa, huku akisisitiza kuwa kiingilio kwenye mchezo huo kitakuwa bure kwa mashabiki wote.
‎Katika mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga alitoa hamasa kwa wananchi kuujaza uwanja wa Kambarage, jambo ambalo liliwezekana. 
‎Aidha, aliahidi zawadi ya shilingi milioni moja kwa kila bao litakalofungwa na Stand United.
‎Mashabiki wa soka wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kesho Julai 8, 2025, kushuhudia Fountain Gate wakipambana kuhakikisha wanasalia kwenye Ligi Kuu huku Stand United wakisaka nafasi ya kupanda.

Post a Comment

0 Comments