Na John Walter-Kondoa
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, Ashatu Kijaji, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo iliyotekelezwa katika jimbo hilo.
Akizungumza mbele ya Rais Samia wakati wa mkutano wa kampeni mkoani Dodoma, Kijaji alisema Kondoa Vijijini imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
“Huduma za afya ambazo zamani zilikuwa changamoto kubwa, sasa tumepata vituo vya afya sita na cha saba kikiwa katika ujenzi, vilevile, tumekamilisha hospitali ya kisasa ya halmashauri ya Kondoa Vijijini yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5,” alisema Kijaji.
Aidha, alieleza kuwa zaidi ya visima 100 vya maji vimechimbwa na kuondoa tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wananchi, wakati barabara na madaraja mbalimbali yamejengwa ili kurahisisha shughuli za uchumi na usafirishaji.
Kijaji aliongeza kuwa hadi sasa vijiji 84 na vitongoji 221 vya jimbo hilo vinaunganishwa na umeme, jambo ambalo limechochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumzia changamoto za baadhi ya watu kupuuza mafanikio hayo, Kijaji alisema: “Ninashangaa kuona wachache wasio na shukrani wakidai hakuna kilichofanyika, wakati ushahidi wa maendeleo upo wazi.”
Pia alimshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumteua kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri serikalini, akiahidi kuendelea kuwa mwaminifu, mwadilifu na kushirikiana na wananchi wa Kondoa kusukuma gurudumu la maendeleo.
Kijaji alihitimisha kwa kusema kuwa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Rais Samia, wananchi wa Kondoa Vijijini hawana budi kumpa kura za kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
0 Comments