F RC Manyara Ataka Jamii Kulea Watoto kwa Upendo Ili Kukomesha Ukatili | Muungwana BLOG

RC Manyara Ataka Jamii Kulea Watoto kwa Upendo Ili Kukomesha Ukatili

Na John Walter-Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinawajengea tabia ya kuwa wakatili wanapokuwa wakubwa, hali inayozorotesha malezi bora katika jamii.

Akizungumza kwenye kongamano la elimu, malezi na ukatili wa kijinsia lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Manyara, Mhe. Sendiga aliitaka jamii kuhakikisha watoto wanalelewa kwa upendo ili wakikua wawe na mioyo laini na mepesi.

Amesema mkoa wa Manyara unaendelea kufanya jitihada kubwa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. 

Aidha, alihoji uwezekano wa baadhi ya kina baba wanaochelewa kurejea nyumbani au kuamua kuwa na uhusiano nje ya ndoa, kama ni matokeo ya ukatili wanaoupitia majumbani mwao.

“Malezi bora ni msingi wa familia na jamii yenye mshikamano. Tukiwalea watoto kwa hofu na ukatili, tutakuwa tunakuza kizazi cha wakatili,” alisema Sendiga.

Kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa CCM mkoani Manyara likiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu malezi na kupinga ukatili wa kijinsia.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Manyara, Ndg. Christina Masagasi, amewataka wadau kuendelea kupambana na vitendo vyote vinavyokiuka haki za binadamu na kuhakikisha watoto wanalindwa bila ubaguzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Ndg. Janes Darabe, amesema kongamano hilo limekuwa na umuhimu mkubwa kwani limehusisha walimu pamoja na makada wa CCM kutoka wilaya zote za Mkoa wa Manyara.


Post a Comment

0 Comments