F Airtel Yaendeleza Elimu Kidijitali Kupitia Vifaa vya Intaneti ya Bure Mkoani Mbeya | Muungwana BLOG

Airtel Yaendeleza Elimu Kidijitali Kupitia Vifaa vya Intaneti ya Bure Mkoani Mbeya


Airtel Tanzania imedhihirisha dhamira yake ya kuleta usawa katika elimu ya kidijitali kwa kukabidhi vifa vya kujifunzia vyenye uwezo wa intaneti kwa shule za sekondari za serikali mkoani Mbeya, kupitia mpango wa kitaifa wa SmartWASOMI.

Mchango huu ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kuharakisha mabadiliko ya elimu kupitia miundombinu ya intaneti, vifaa vya kisasa, pamoja na upatikanaji wa bure wa maudhui ya kielimu yanayokidhi mtaala wa taifa.

Mpango wa SmartWASOMI unaunga mkono kwa vitendo Mkakati wa TEHAMA kwenye Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, sambamba na vipaumbele vya sera ya TEHAMA ya mwaka 2025/26 ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti na ujuzi wa kidijitali katika shule za sekondari nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Msimamizi wa Teknolojia kutoka Airtel Tanzania, Bw. Harrison Isdory, alifafanua kuwa SmartWASOMI ni suluhisho jumuishi linalochanganya huduma ya intaneti, vifaa vya kisasa na maudhui rasmi ya kujifunzia:

“Mpango huu hauishii kwenye intaneti tu; unahakikisha pia upatikanaji wa vifaa pamoja na maudhui yaliyoandaliwa yanalingana na mitaala ya elimu nchini. Vifaa vilivyotolewa vina uwezo wa kutumia intaneti ya kasi na vimeandaliwa kubeba maudhui kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) pamoja na majukwaa mengine kama Shule Direct, yote haya bila gharama ya data kwa watumiaji wa mtandao wa Airtel.”

Kila kifaa kimetayarishwa tayari kwa matumizi ya kielimu, kikiwa na maudhui yaliyoratibiwa na yanayopatikana bila matumizi ya data, hivyo kuwaondolea walimu na wanafunzi changamoto ya gharama kubwa za intaneti katika mazingira ya kujifunzia.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mbeya Day, Bw. Titus Oscar, aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Sekondari Mkoa wa Mbeya, aliipongeza Airtel kwa kupanua mpango wa SmartWASOMI na kuzifikia shule za umma mkoani humo:

“Hili ni tukio la kihistoria kwa mkoa wa Mbeya. Tunashuhudia namna Airtel inavyobadilisha taswira ya elimu kupitia teknolojia. Kupitia vifaa hivi vyenye intaneti ya kasi, wanafunzi wetu sasa wanaweza kupata rasilimali za kidijitali kwa masomo yao yote. Hii inaleta hamasa mpya darasani na kuwaandaa wanafunzi kwa dunia ya sasa inayotegemea sana TEHAMA.”

Mmoja wa walimu kutoka shule ya Sekondari Kaloge, Samwel Mdengede alisema, “Kabla ya msaada huu, mazingira ya kidijitali shuleni kwetu yalikuwa duni sana. Kupitia vifaa hivi, tunaweza kuendesha masomo kwa kutumia kupitia mfumo wa kujifunza kielektroniki yaani e-learning, kufanya utafiti, na kufundisha sayansi na hisabati kwa njia shirikishi zaidi. Hii ni nyenzo muhimu ya kuboresha matokeo ya elimu.”

Kutoka shule ya Legiko, Mwalimu Elice mwakabage aliongeza kuwa, “Kuingiza TEHAMA kwenye ufundishaji ni hatua muhimu ya kuwaandaa wanafunzi kwa masomo ya juu na ajira za siku zijazo. Vifaa hivi si tu vinatoa maudhui ya masomo, bali vinajenga pia ujuzi wa msingi wa kidijitali ambao ni muhimu kwa maisha ya baadaye.”

Utekelezaji wa mpango huu mkoani Mbeya ni mwendelezo wa mkakati wa kitaifa wa SmartWASOMI ambao tayari umefikia shule katika mikoa ya Zanzibar, Arusha, Kilimanjaro, Tabora, Dodoma na maeneo mengine. Mpango huu unajumuisha uwekaji wa miundombinu ya intaneti, usambazaji wa vifaa, pamoja na mafunzo kwa walimu ili kuhakikisha matumizi bora na endelevu ya TEHAMA katika elimu.

Kwa kushirikiana na UNICEF na Wizara ya Elimu, Airtel Tanzania inalenga kuunganisha shule 3,000 za sekondari za serikali nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano. Mpango huu unahusisha tathmini ya kiufundi kwa shule, upangaji wa miundombinu, mafunzo kwa walimu juu ya matumizi ya vifaa vya kidijitali, na msaada wa kiufundi wa muda mrefu ili kuhakikisha uendelevu wa mfumo huo.

Kupitia mchango huu wa karibuni mkoani Mbeya, Airtel inaendelea kudhihirisha kwamba ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali unaweza kuleta suluhisho la kweli, lenye gharama nafuu na linalofikia wengi kwa ajili ya kuleta usawa wa kidijitali katika elimu ya Tanzania.



Post a Comment

0 Comments