F Dkt Samia Aagiza Mabalozi wa CCM Kuhakikisha Wananchi Wote Wanapiga Kura Oktoba 29 | Muungwana BLOG

Dkt Samia Aagiza Mabalozi wa CCM Kuhakikisha Wananchi Wote Wanapiga Kura Oktoba 29


Na John Walter, Babati

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa agizo kwa mabalozi wote wa CCM kuhakikisha kila mwananchi aliyejiandikisha kwenye daftari la mpiga kura anatoka kwenda kupiga kura siku ya Oktoba 29.

Amesema hata kama kuna mgonjwa, ipo kamati maalum ya kusaidia wananchi hao ili kuhakikisha kila mmoja anatimiziwa haki yake ya kikatiba ya kupiga kura.

Dkt. Samia alitoa agizo hilo leo tarehe 4 Oktoba 2025, wakati akinadi Ilani ya CCM ya mwaka 2025/30 pamoja na sera na ahadi zake mbele ya maelfu ya wananchi wa Babati, mkoani Manyara, katika muendelezo wa mikutano yake ya kampeni.

Akizungumza kwa msisitizo, Dkt. Samia aliwaomba wananchi kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi na kukipa ridhaa ya kuongoza nchi kwa kipindi kijacho, akisema:

“Tupeni kazi CCM tukaulinde na kuendelea kuujengea heshima utu wa kila Mtanzania na kwa maendeleo endelevu.”

Aidha, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa wananchi kutofanya makosa ya kuchanganya viongozi watakaowachagua, akiwataka kushikamana na CCM kwa mafiga matatu ambayo ni Rais, Mbunge na Diwani.

“Tunawaomba kura zenu wananchi wote—kwangu mimi kwa nafasi ya Rais wa Tanzania, kwa Wabunge na Madiwani wote wanaotokana na CCM. Nawaomba sana msije mkawachanganya, kwa kuwa wakiongea kwa sauti moja, maendeleo yatakwenda haraka,” alisema.

Dkt. Samia pia alihusisha taswira yake kwenye mabango na karatasi za kura, akiwahakikishia wananchi kuwa kura wanazoziona kwenye picha ndiyo sura ile ile wakienda kupiga kura.

Ziara ya kampeni ya Dkt. Samia katika mkoa wa Manyara imeendelea kuvuta maelfu ya wananchi, ambapo wananchi wameahidi kuipa CCM kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Post a Comment

0 Comments