Na John Walter-Hanang'
Mgombea ubunge wa Jimbo la Hanang’ kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Asia Halamga, amemuomba mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha wilaya hiyo inajengewa kiwanda cha nafaka ili vijana wapate ajira na kuinua uchumi wa wananchi.
Asia ametoa ombi hilo leo Oktoba 3, 2025, wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mlima Hanang’, Katesh, alipokuwa akiomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
“Hapa Hanang’ tuna mazao ya kilimo na pia chumvi, tunakuomba Mama Samia utujengee viwanda ili wananchi wapate ajira na kukuza kipato chao,” alisema Asia.
Ameongeza kuwa wilaya hiyo tayari ina huduma bora za kijamii, ikiwemo elimu na afya, hivyo kipaumbele kwa sasa ni uwekezaji kwenye viwanda ili kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana.
Katika mkutano huo, Asia amemwahidi Dkt. Samia kuwa wananchi wa Hanang’ wapo tayari kumpa kura nyingi za ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara, Peter Toima, amemhakikishia mgombea wa urais kuwa chama hicho kitapata kura zote kwa asilimia 100 kutoka mkoani humo.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amesema ana imani kuwa wananchi wa Manyara, hususan Hanang’, watampatia Dkt. Samia kura zaidi ya asilimia 90 kutokana na imani kubwa waliyonayo kwake na katika chama cha Mapinduzi.
0 Comments