Serikali imesema inaendelea kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa wadau wa sekta ya kilimo nchini, hususan kampuni za PASS Leasing na KANU Equipment, ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kusogeza huduma za teknolojia ya kisasa kwa wakulima ili kuongeza tija kwa gharama nafuu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almish Hazal, wakati wa hafla ya kukabidhi matrekta 20 kwa wakulima pamoja na kuzindua ofisi ya KANU Equipment katika mji mdogo wa Katesh, mkoani Manyara.
Amesema serikali inaunga mkono jitihada za wadau hao ambazo zinalenga kumuwezesha mkulima mdogo kufanya kilimo cha kisasa na cha kibiashara, jambo litakalosaidia kuongeza kipato cha kaya na pato la taifa kwa ujumla.
“Mikopo hii ya zana za kilimo yenye masharti nafuu itasaidia kuongeza uzalishaji, hivyo niwasihi wakulima wote kutumia vizuri fursa hii na kurejesha mikopo kwa wakati,” amesema Hazal.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PASS Leasing, Killo Lusewa, amesema kampuni hiyo imeendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu bila dhamana kwa wakulima, wavuvi na wafugaji yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 70, huku wilaya ya Hanang’ pekee ikinufaika na mikopo ya zaidi ya bilioni 15.
Amesema mazingira mazuri ya kisera na utawala bora nchini yameiwezesha PASS Leasing kufanya kazi kwa ufanisi na kufanikisha zoezi la kukabidhi matrekta 20 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 kwa wakulima wa Hanang’.
“Tunawaomba wakulima waendelee kuwa waaminifu katika kurejesha mikopo hii ili iweze kuwasaidia wengine pia,” amesema Lusewa.
Mnufaika wa mpango huo, Marko Momoya, amesema trekta alilopokea litamsaidia kulima hekari 30 alizonazo kwa urahisi zaidi na kupunguza gharama za uzalishaji.
“Kampuni ya PASS Leasing inamsikiliza mteja hata wakati wa changamoto za marejesho, hivyo nawaomba wakulima wenzangu wasiwe na hofu,” amesema Momoya.
Naye Meneja Biashara wa PASS Leasing Kanda ya Kaskazini, Maria Wambura, amesema kampuni hiyo imekuwa ikiendelea kusaidia wakulima wa Hanang’ kila mwaka ambapo mwaka 2021 walikabidhi matrekta 20, mwaka 2023 walitoa 10, na mwaka huu 2025 wameongeza mengine 20.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Daniel Luther, amesema wilaya hiyo ni miongoni mwa nguzo muhimu za kilimo nchini kwani ina zaidi ya wakulima 400 wanaotumia matrekta na zana nyingine za kilimo zaidi ya 200.
Ameongeza kuwa kufunguliwa kwa ofisi ya KANU Equipment Katesh kutarahisisha huduma za matengenezo na upatikanaji wa vipuri bila wakulima kulazimika kusafiri hadi Arusha au Babati.
“Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu kufanya kilimo cha kisasa kwa urahisi zaidi na kuongeza uzalishaji,” amesema Luther.
0 Comments