F Peter Toima: Wana Manyara tumejipanga Kuipa CCM Ushindi Uchaguzi Mkuu | Muungwana BLOG

Peter Toima: Wana Manyara tumejipanga Kuipa CCM Ushindi Uchaguzi Mkuu




Na John Walter-Hanang'

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Peter Toima, amesema wananchi wa mkoa huo wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu na kuhakikisha wanampa kura nyingi mgombea wa chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wengine wa CCM.

Toima ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara wa kampeni za mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika mkoani Manyara na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Amesisitiza kuwa wananchi wa Manyara wanatambua kazi kubwa iliyofanywa na Dkt. Samia katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo miradi ya miundombinu, elimu, afya na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

“Wana Manyara tumeshajipanga, tunakwenda kumhakikishia Dkt. Samia kura za kishindo Oktoba 29. Tuna imani naye na tunajua CCM ndicho chama pekee chenye dira ya kweli ya maendeleo kwa Watanzania,” alisema Toima huku akishangiliwa na wananchi.

Kwa upande wake, Dkt. Samia amewashukuru wananchi wa Manyara kwa mapokezi makubwa na kuahidi kuendelea kusimamia maendeleo ya taifa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza kwa muhula mwingine.

Mkutano huo wa kampeni ulipambwa na shamrashamra mbalimbali, ikiwemo burudani za muziki na ngoma za kitamaduni, huku wafuasi wa CCM wakiahidi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.



Post a Comment

0 Comments