Na John Walter-Babati
Jumuiya ya SMAUJATA Mkoa wa Manyara, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Shujaa Hassan Kimu, imekemea vikali tabia ya baadhi ya wazazi na viongozi wanaomaliza kesi za ukatili wa kijinsia kienyeji badala ya kuziacha zifuate taratibu za kisheria.
Akizungumza wakati wa mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Chief Dodo, Babati Vijijini, Kimu alisema kuwa vitendo vya ukatili, ikiwemo ubakaji na ulawiti, havitakoma iwapo jamii itaendelea kupokea rushwa na kupoteza ushahidi unaohusiana na kesi hizo.
“Matukio haya hayawezi kukoma kama jamii na viongozi hatutaacha kupokea rushwa na kupoteza ushahidi. Tunapaswa kusimama kidete kulinda haki za waathirika na kuhakikisha wanaofanya ukatili wanawajibishwa ipasavyo,” alisema Kimu.
Aidha, SMAUJATA mkoa wa Manyara imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kampeni za kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kuripoti matukio hayo kwa mamlaka husika.
“Tunataka ujumbe huu uwafikie wote — ukatili sio siri, sio aibu, ni kosa la jinai,” alisisitiza Kimu.
Kwa upande wake Mgombea udiwani (CCM) Kata ya Riroda, Mheshimiwa Nyangweli, amesema kuwa katika historia ya eneo hilo matukio ya ubakaji na ulawiti hayakuwepo, hivyo kushangazwa na ongezeko la visa hivyo kwa sasa.
“Jamii yetu inapaswa kuamka. Vitendo vya ukatili havina nafasi, na wanaofanya vitendo hivyo wanastahili kufungwa hata maisha,” alisema Nyangweli.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, viongozi wa serikali za mitaa, walimu na wanafunzi, huku ujumbe mkuu ukiwa ni kuendeleza ushirikiano katika kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.
0 Comments