Na Timothy Itembe Tarime.
WAANDISHI wa habari kutoka mikoa mbalimbali nchini, wakiwemo kutoka Mkoa wa Mara, wamejengewa uwezo juu ya namna ya kuandika na kuripoti habari zinazohusu ukatili wa kijinsia kwa njia ya kitaalamu, inayolinda utu na faragha ya waathirika pamoja na jamii kwa ujumla.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika katika Hoteli ya CMG wilayani Tarime, yamelenga kuwawezesha waandishi kuandika habari zenye kuelimisha, kuleta mabadiliko chanya, na kuepuka lugha au maudhui yanayoweza kuchochea upya maumivu ya kihisia kwa waathirika.
Akizungumza katika mafunzo hayo, mwezeshaji wa semina hiyo, Bi. Victa Maleko, alieleza umuhimu wa waandishi kuzingatia kanuni ya msingi ya “kutokusababisha madhara zaidi” wakati wa uandishi wa habari zinazohusu ukatili wa kijinsia.
“Kanuni hii inasisitiza kuwa msaada wowote unaotolewa haupaswi kuongeza madhara, iwe ya kimwili, kiakili au kijamii. Ni muhimu kwa waandishi kuweka kipaumbele katika kulinda usalama, heshima na faragha ya waathirika,” alisema Maleko.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime,Siwema Atieno Selevesta, ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Chaguo Langu, Haki Yangu, unaofadhiliwa na Shirika la Idadi ya Watu Duniani UNFPA alisema kuwa mradi huo umeleta mabadiliko chanya kwa jamii kwa kushirikisha makundi mbalimbali, yakiwemo wanawake, watoto, wanaume na watu wenye ulemavu.
“Mradi huu umesaidia kuongeza uelewa katika jamii kuhusu namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia Watu sasa wanafahamu wapi pa kuripoti, na wamekuwa wakitumia huduma kama vile kupiga simu namba 116 – huduma ya bure kwa mtoto, inayoratibiwa na Shirika la SISEMA chini ya mradi wa Haki Yangu, Chaguo Langu,” alifafanua Selevesta.
Washiriki wa semina hiyo wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa mbinu bora za kiuandishi zitakazosaidia kuandika habari zenye kuhamasisha mabadiliko katika jamii bila kuongeza madhara kwa waathirika.
“Tumekumbushwa kuandika habari zenye mwelekeo chanya. Tusiwe waandishi wanaoongeza matatizo juu ya matatizo. Tunapaswa kusaidia, si kuumiza zaidi kwa kuandika kwa namna isiyofaa,” alisema Esther Baraka, mshiriki kutoka Mwanza.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za kuimarisha vyombo vya habari kama washirika muhimu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuendeleza jamii yenye usawa, heshima na haki kwa wote aliongeza Baraka.
0 Comments