Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa jana amerejesha fomu ya
kuwania urais, huku akifanikiwa kupata wadhamini milioni 1.6, zaidi ya nusu ya
kura za urais ambazo chama hicho kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar , Salum Mwalimu alisema idadi hiyo ya
wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa maelezo kuwa inakaribia idadi ya
kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipogombea
urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Katika Uchaguzi huo, Dk Slaa alishika nafasi ya pili baada
ya kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34, huku Rais Jakaya Kikwete
akipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Lowassa alipochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais
kwa tiketi ya CCM, kabla ya kuhamia Chadema, alidhaminiwa na wanachama 870,000
nchi nzima.
Dk Slaa, ambaye hajaonekana hadharani tangu Lowassa ajiunge
Chadema, jana hakuwapo kwenye ofisi za chama hicho wakati mbunge huyo wa
Monduli alipokuwa akirejesha fomu.
Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala lake,
lakini baadhi ya maofisa wa Chadema walisema wanaendelea kuchapa kazi.
Katika hafla ya jana, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara,
Profesa Abdallah Safari alieleza jinsi Chadema ilivyojipanga kuchukua nchi na
siyo kushinda ubunge na udiwani pekee na kwamba Lowassa amebakiza hatua mbili
tu kuingia Ikulu, jambo walilodai kuwa limeichanganya CCM.
Wakati Lowassa ambaye alitangaza rasmi kujiondoa CCM na
kujiunga na Chadema Julai 28 mwaka huu akisubiri kupitishwa na Mkutano Mkuu wa
chama hicho utakaofanyika Agosti 4, habari za ndani zinaeleza kuwa vigogo kadhaa
wa CCM watatambulishwa katika mkutano huo.
Habari hizo zinaeleza watakaotambulishwa siku hiyo ni
wenyeviti wa CCM wa mikoa, wilaya na waliokuwa wabunge wa chama hicho ambao
wanamuunga mkono Lowassa.
Jana Lowassa, aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi
na aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser VX, alifika makao makuu ya
Chadema saa 9:35 alasiri akiwa pamoja na familia yake na alipokewa na umati
mkubwa wa watu waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Baadhi ya ujumbe huo ni “Chini ya Lowassa umaskini haupo”,
“Kwa Lowassa hata maskini atapata ajira” na “Kingunge Ngombare-Mwiru karibu
Ukawa”. Kingunge ni kada mkongwe wa CCM na anamuunga mkono Lowassa.
Mbali na kubeba mabango, watu hao walikuwa wakiimba nyimbo
mbalimbali za kumsifu Lowassa na kushangilia pale ilipokuwa ikitajwa mikakati
ya chama hicho kushika dola.
Akieleza taratibu na kanuni za kudhamini mgombea urais,
mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira alisema
mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama wasiopungua 200.
“Naamini fomu za
Lowassa zitakuwa na idadi hiyo ya wadhamini. Ila baada ya mgombea kuchukua fomu
jioni yake wanachama wa Chadema, wapenzi na Watanzania walifurika katika ofisi
za Kanda, mikoa na majimbo nchi nzima wakiomba kumdhamini,” Kigaira.
Alisema wanachama hao walidhani fomu hizo zimepelekwa kila
mkoa, kutokana na kuepuka kuwanyima fursa hiyo chama hicho kilipeleka fomu ili
wanachama wamdhamini na kupewa masharti kuwa lazima wawe wamejiandikisha kupiga
kura, wataje namba zao za simu.
