Kwenye baadhi ya maeneo kazi hiyo iliahirishwa hadi leo
kutokana na vifaa kuchelewa na pia tatizo la kugundulika kwa shahada ambazo
zimeshapigwa kura zikiwa ndani ya maboksi.
Lakini matukio yaliyotawala kura za maoni ni makada
kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kugawa fedha au
kuchapisha karatasi bandia za kupigia kura.
Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam , Takukuru inawashikilia
wagombea sita kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe ili wachaguliwe kwenye
kura za maoni.
Makamu mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni, Denis Manumbu
aliwataja waliokamatwa kuwa ni katibu wa kata ya Kibamba, Denisi Kalela, katibu
wa itikadi, Babu Kimanyo, diwani wa viti maalumu wa Goba, Rehema Luhanja,
Wengine ni mwenyekiti kata ya Goba, Pili Mustafa, mgombea
udiwani, Msigani Mwasha na Eliasi Nawera ambaye anagombea ubunge Jimbo la Kawe.
Alisema kuwa Kalela, na Kimanyo walikamatwa juzi saa 4:00
usiku maeneo ya Kibamba CCM, huku Mustafa na Luhanja wakikamatwa maeneo ya Goba
Kati na Kawe.
“Walikamatwa wakiwa wanatoa rushwa na wengine walikamatwa
wakiwa na kiasi cha pesa ambazo bado walikuwa wanazigawa huku wengine
wakiwashawishi wajumbe kupokea rushwa,” alieleza Manumbu.
Manumbu alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi ofisi yao inafanya kazi saa 24
ikipokea taarifa zote zinazohusu rushwa.
Kondoa
Lakini hali ilikuwa mbaya wilayani Kondoa, Dodoma ambako CCM ililazimika kuchoma moto
makasha sita ya kupigia kura baada ya kubainika kuwa baadhi ya wanachama
walitumia kadi ya CCM pekee bila ya kitambulisho cha kupigia kura.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Shaaban Kissu, mwenyekiti wa CCM
wa wilaya, Othman Gora na kamanda wa polisi wa wilaya, Nyantora walikubaliana
kuchomwa moto baada ya kubaini tatizo hilo .
Hatua hiyo, inatokana na wanachama kuanzisha zogo kuwa
vitambulisho vya kura havikutumika kabla ya uamuzi huo kufikiwa. Tayari zaidi
ya wanachama 200 walikuwa wamepiga kura hizo.
Maboksi hayo yalichomwa mbele ya kituo cha kupigia kura cha
Ubembeni na kushuhudiwa na wananchi, wananchama wa CCM, polisi na uongozi wa
CCM.
Baada ya kuyachoma, Kissu alitangaza kuahirishwa kwa
uchaguzi huo baada ya dosari hiyo na kwamba utarudiwa leo.
Baadaye kamanda wa polisi wa wilaya aliamrisha watu wote
kutawanyika eneo hilo
hadi leo.
Awali kulitokea vurugu baada ya baadhi ya wanachama kunyakua
sanduku lililokuwa na kura na kutaka kukimbia nalo kwa tuhuma kuwa mawakala
hawakuwa wakitenda haki kwa wapiga kura
Mbeya
Kashfa ya matumizi ya rushwa pia ilijitokeza mkoani Mbeya
ambako mgombea udiwani mmoja kulalamikiwa kwa madai ya kuwakodisha wanafunzi
wampigie kura kwa malipo ya Sh2,000 kwa kila mmoja.
Mgombea huyo wa udiwani wa Kata ya Mbalizi Road analalamikiwa pia alikwenda
kwenye kilabu za pombe kuwatafuta watu wanaotaka kumpigia kura ili awanunulie
kinywaji.
Miongoni mwa walalamikaji ni Ally Salum na Aziza Mbika wa
eneo la Sabasaba ambao walisema walimwona mgombea huyo akitoa fedha na pombe
kwa vijana mbalimbali .
Msimamizi wa uchaguzi wa Kituo cha Meta ,
Ndoni Mwakalukwa alikiri kupokea malalamiko ingawa hakushuhudia utoaji wa fedha
hizo na kwamba atayazungumza baada ya kumaliza kazi ya upigaji kura.
Vituo vingine, vikiwamo vya Kata za Ruanda
na Sinde, vilikosa wanachama wa kupiga kura na badala yake walifika mmoja mmoja
kila baada ya saa kupita.
Wasimamizi wa uchaguzi maeneo hayo walikuwa na kazi ngumu ya
kuwaita watu waliokuwa wakipita wakiwaomba wakapige kura kama
ni wanachama wa CCM.
“Tatizo ni kwamba vituo vya kupigia kura havijawekewa alama
yoyote, hivyo wanachama wengi hawajui,’’ alisema msimamizi wa kituo cha Soweto , Ambakisye Kitunga.
Lindi
Rushwa pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Mchinga (CCM) ambako
mbunge wa viti maalumu, Fatuma Mikidadi alikamatwa na Takukuru kwa tuhuma za
kutoa rushwa kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo waliomkamata kwa tuhuma za hongo.
Habari zinasema kuwa mgombea huyo alikutwa na wafanyakazi wa
Takukuru akitoa rushwa kwa wanachama wa Kata ya Mchinga.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mikidadi alikasirika
akisema: “Uongo, uongo, huu ni uzushi kabisa.”
Alipoulizwa kwa nini anafikiri wamemsingizia, alisema:
“sijui hawa wanasingizia singizia tu, uongo.” Hata hivyo, kamanda wa Takukuru
wa mkoa wa Lindi, Steven Chami alisema Fatuma alikamatwa saa 5:00 usiku Kata ya
Mchinga akigawa fedha kwa wanachama.
Chami alisema akiwa ofisi za Takukuru baada ya mahojiano,
mtuhumiwa huyo alitoa tena Sh780,000 kwa ajili ya kuwahonga maofisa hao ili
wasiendelee na suala hilo .
Alisema kutokana na kitendo hicho, Takukuru itamfikisha
mahakamani muda wowote baada ya mwanasheria kutafsiri na kubainisha tuhuma
zake.
Wakati huohuo, kamanda huyo alisema mgombea ubunge wa Jimbo
la Lindi Mjini, Mohamedi Utali alishikiliwa kwa muda wa saa kadha kwa mahojiano
na Takukuru baada ya kukutwa na Sh4milioni saa 8:30 usiku akiwa Kata ya Mbanja.
Chami alisema kukamatwa kwa mgombea huyo kulitokana na
ushirikiano baina ya wananchi na taasisi hiyo.
Shinyanga
Mjini Shinyanga, katibu wa Kata ya Mjini Shinyanga,
Ramadhani Majani amenusurika kipigo baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia jana
akiwa ofisini kwake na mmoja wa wagombea udiwani na ubunge katika Jimbo la
Shinyanga Mjini.
Mashuhuda wa tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari jana
kwamba Majani alikutwa na kadhia hiyo baada ya watu waliotilia shaka nyendo
zake kwa kitendo chake cha kuongozana na mmoja wa wagombea nyakati za usiku
kuingia ofisini na hivyo kuhisi kuna jambo lisilokuwa la kawaida walilopanga
kufanya.
Walisema waliamua kuwapigia simu wagombea wengine
waliokwenda ofisi hizo na kumkuta mgombea mmoja (jina limehifadhiwa) akiwa
anaongea naye, hata hivyo walishituka ghafla baada ya kuona kundi la wana-CCM
wakijongea ofisini hapo.
“Sisi tulipigiwa simu usiku saa 4:45 na baadhi ya watu
wanaoishi jirani na ofisi yetu ya kata kwamba wamemuona katibu kata wetu akiwa
na mgombea udiwani pamoja na wapambe wake. Walidai inavyoelekea walikuwa
wakipanga mikakati mibovu ya kutaka kuiba kura,” alisema Rashidi Abdalah.
“Taarifa hizo zilitushangaza sana . tuliamua kuchukua gari na kwenda katika
eneo la ofisi na kweli tulimkuta katibu kata akiwa na mgombea (anamtaja jina)
wakiwa nje ya ofisi za CCM wakitaka kuingia ndani, ghafla walipotuona mgombea
na wapambe wake walikimbia na katibu kata aliingia ofisini na kuufunga mlango,”
alieleza aliongeza.
Abdalah alidai kitendo cha Majani kukimbilia ofisini
kilisababisha baadhi ya watu kushikwa na hasira na kutishia kuvunja mlango ili
kumtoa nje na kumshushia kipigo, lakini mgombea
mwingine alimsihi ajisalimishe na kufanikiwa kutuliza
ghasia.
Majani alikiri kutaka kupigwa na kundi la wana-CCM na kwamba
ni kweli muda huo wa usiku alikuwa ofisini akifanya kazi ya kugonga muhuri
kwenye karatasi za kupigia kura japo hakuweza kufafanua kitendo cha mmoja wa
wagombea kuwa katika maeneo hayo nyakati hizo za usiku.
“Nilikuwa naendelea na kazi zangu lakini baadaye nilishangaa
watu wanakuja na fimbo wakidai niko na mgombea ilibidi nijifungie ofisini
kwangu,” alisema Majani.
Handeni
Hali ya sintofahamu ilitanda kwenye tawi la Bomani, Kata ya
Vibaoni wakati zaidi ya wanachama 60 walipogoma kupigia kura wagombea udiwani
kwa maelezo kuwa hawawafahamu kwa kuwa hawakufika eneo hilo kujinadi na badala yake kuamua kupiga
kura ya wagombea ubunge.
Wakizungumza jana wakati wa kuwasubiri wagombea, wanachama
hao walisema kuwa walikutana kuanzia saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kuwasubiri,
lakini hawakutokea hadi saa 12:00 jioni, kitu ambacho walidai kuwa ni dharau.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani, John Mohamed alisema kuwa
walikubaliana kukutana na madiwani hao kwa mara ya kwanza, lakini akidi ya
wanachama haikutimia ikawabidi kuahirisha kikao hicho hadi jana lakini kitu cha
ajabu wagombea hao hawakutokea hadi jioni.
Arusha
Sakata la karatasi bandia za kupigia kura pia liliibuka
mkoani Arusha, ambako viongozi wawili wa CCM walikamatwa kwa tuhuma hizo.
Waliokamatwa ni katibu wa Kata ya Mjini Kati, Ally Meku na mwenyekiti wa Mtaa
wa Bondeni, Yakub Shaban.
Katibu wa Wilaya ya Arusha, Feruz Bano alisema: “Ni kweli
wamekamatwa, lakini tunafuatilia kujua kosa lao kwa kuwa hawana ofisi, hivyo
walikuwa wanapeleka karatasi hizo kwenye chumba cha kupigia kura kidogo
kidogo,” alisema.
Rafu iligubika uchaguzi huo mkoani Dodoma ambako baadhi ya wanachama walikamatwa
na shahada bandia, huku vurugu zikiripotiwa maeneo kadhaa.
Waliokamatwa na tuhuma kuwa walikuwa na shahada bandia ni
katibu wa vijana Tawi la Chang’ombe, Nasra Salum akiwa na shahada 20 za kupigia
kura, 20 za udiwani, Bakari Fundikira (za ubunge), na David Malolle.
Mwingine aliyekamatwa kwa tuhuma hizo ni Faisi Mussa ambaye CCM
imeeleza alikutwa na shahada 15 bandia.
Aidha, baadhi ya kata zilishindwa kufanya uchaguzi kutokana
sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na karatasi za kupigia kura kuwa
na makosa. Miongoni mwa kata zilizoshindwa kufanya uchaguzi huo ni Tambukareli
na Kilimani mjini Dodoma .
Katibu wa CCM wa mkoa, Albert Mgumba alisema kata ambazo
hazijafanya uchaguzi, kazi hiyo itafanyika leo kabla ya saa 4:00 asubuhi.
Kuhusu makada waliokamatwa, katibu huyo alisema jambo hilo waulizwe makatibu wa wilaya kwa kuwa
ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, vurugu zimetokea katika tawi la Mji
Mpya lililoko Kata ya Uhuru kutokana na baadhi ya wanachama kudai kuna mamluki
wameingia kupiga kura.
“Asubuhi walikuja watu kutoka Tawi la Uhuru wakidai kuwa kuna
mamluki wanataka kupiga kura kwenye tawi letu, lakini baada ya viongozi kufika
tulirekebisha na zoezi likaendelea kwa amani na utulivu,” alisema msimamizi wa
kituo hicho, Mariam Jumbe.
Bukoba
Hali ilikuwa tofauti mkoa Kagera ambako uchaguzi huo majina ya
wanachama waliofariki dunia yalikuwapo kwenye orodha ya wapiga kura Jimbo la
Nkenge huku kukiwa na hofu ya kuanguka kwa vigogo.
Hali hiyo ilitokea katika vituo vya Mutemba na Igayaza. Hata
hivyo, katibu wa CCM wa Wilaya ya Missenyi, Mwajuma Mboha alisema kujulikana
kwa majina hayo, ni matunda ya uwepo wa mawakala katika uchaguzi huo.
Pia kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa majina ya baadhi ya
watu waliofika kupigakura. Katika kata hiyo ya Nsunga kulikuwa na watu saba
waliolalamikia kutoorodheshwa.
Mtwara
Kukosekana kwa majina katika orodha ya wapigakura pia
ilijitokeza kwenye Manispaa ya Mtwara Mindindani.
Wakiongea na Mwananchi, Shangani Aisha Ismail na Salima
Nassoro wa Tawi la Vigaeni walisema wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa CCM
kuwapa kadi za chama bila kuweka majina yao
katika daftari la wapigakura.
“Sisi tumepewa kadi tunazo mikononi hatujui kama nyingine zimesajiliwa au la. Nyingine tumezilipia na
majina yetu hayapo. Kuna kadi nyingine za mwaka 2000 hadi mwaka 1950 zipo na
majina yao yapo na sisi majina yetu hayapo kuna nini hapa?” alihoji Aisha
Katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya, Mohamed Watanga
alikiri kuwapo na tatizo hilo ,
akieleza kuwa wanalitafutia ufumbuzi.
Njombe
Pia mkoani Njombe, wanachama walishindwa kupigakura kutokana
na kadi zao za uanachama kuonekana kuwa zilikatwa baada ya Julai 15, siku
ambayo CCM ilifunga kazi ya kuandikisha wanachama wapya.
Msimamizi wa uchaguzi wa kituo cha Mpechi, Sarah Nyandoa
alisema licha ya uchaguzi kufanyika kwa amani, alikiri kuwapo kwa wanachama
waliokuwa na kazi walizopata baada ya Julai 15.
“Ni kweli kuna baadhi ya watu wanakuja na kadi zao
zilizochukuliwa baada ya Julai 18, lakini tumewarudisha baada ya kuwaelimisha
wameridhika,” alisema Nyadoa.
Pwani
Mchakato kura za maoni umeingia dosari katika vituo kadhaa
baada ya baadhi ya wanachama kukatwa majina yao kwenye daftari la orodha ya wanachama wa
chama hicho.
Mbali ya kuwepo majina yaliyokatwa, pia baadhi ya wanachama
walikutwa wakipiga kura kwa kutumia stakabadhi ya malipo ya wanachama maarufu
badala ya kutumia kadi ya uanachama wa CCM.
Kasoro hizo zilisababisha vurugu kwenye baadhi ya vituo vya
kupigia kura mjini Kibaha na kumlazimu mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid
Bundala kusitisha uchaguzi huo kwenye vituo kadhaa vilivyokua na kasoro.
Bundala alisema jana mchana kuwa vituo vilivyofutiwa kufanya
uchaguzi ni Morning Star na Machinjioni vilivyoko Kata ya Tangini mjini Kibaha.
Uchaguzi huo utarudiwa leo.
Alipoulizwa sababu za kuwepo tofauti ya idadi ya majina
yaliyomo kwenye daftari la uanachama na idadi ya wenye kadi za chama eneo hilo , alisema wamebaini
kasoro hiyo imesababishwa na baadhi ya mabalozi kutowasajili kwenye daftari la
chama la wapigakura.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wanachama waliokuwa
wakipiga kura Kibaha Mjini wamelalamikia kuwepo rafu katika mchakato wa upigaji
kura wakisema baadhi ya matawi yaliweka orodha kubwa ya wanachama wanaoruhusiwa
kupiga kura ikilinganishwa na idadi ya awali iliyobandikwa kwenye kuta za ofisi
za matawi yao .
Tarime
Mjini Tarime mkoa wa Mara, uchaguzi ulilazimika kuahirishwa
hadi leo baada ya kukamatwa kwa karatasi bandia za kupigia zilizokuwa
zimeshawekewa alama ya ndiyo kwa wagombea wa ubunge Jimbo la Tarime, na Tarime
Mjini.
habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa karatasi hizo
zinazoendelea kukusanywa, zilitengenezwa na mmoja wa viongozi wa wilaya,
Bernard Nyerembe ambaye amekamatwa na kufikishwa Takukuru kwa mahojiano zaidi.
Habari hizo zinasema kuwa karatasi hizo zilikuwa
zichanganywe na karatasi halali baada ya wanachama kupiga kura za maoni.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Rashid Bogomba alithibitisha
kukamatwa kwa karatasi hizo jana asubuhi.
Alisema kwa Jimbo la Tarime, kura hizo zimekamatiwa katika
vijiji vya Nyamwaga, Masanga na Nyamongo na kwa Jimbo la Tarime Mjini
zimekamatwa Mtaa wa Bomani, Magena na Romori.
Bogomba alisema kutokana na kukamatwa kwa karatasi hizo,
uchaguzi umeahirishwa.
Kamanda wa polisi wa Tarime/Rorya, Benadict Mambosasa pia
alithibitisha kukamatwa kwa Nyerembe na kwamba amepelekwa Takukuru kuhojiwa.
Alisema Nyerembe alikamatwa akiwa ofisi ya CCM ya wilaya baada ya wanachama
kumtuhumu kuwa alikuwa na karatasi zilizokwishapigwa kura kwa ajili ya wagombea
wawili wa majimbo hayo.
Mwananchi ilipomtafuta Nyambari Nyangwine anayetetea ubunge
wa Tarime, na Waziri Gaudensia Kabaka (Tarime Mjini) wote wwalikanusha kuhusika
na kudai hizo ni njama zilizopikwa dhidi yao .
Makada wengine wanaowania ubunge wa Tarime ni Christopher
Kangoye ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nyambari Nyangwine (mbunge), Pius
Marwa, John Gimunta, Maseke Muhono, Lucas Mwita, Paul Matongo na Charles
Machage.
Kwa jimbo jipya la Tarime Mjini wanaogombea ni Waziri wa
Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Maico Kembaki, Philipo Nyirabu, Jonathani
Machango, Ditu Manko na Brito Burure.
