Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inawashikilia makada wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa tuhuma za kujihusisha na utoaji rushwa katika matukio tofauti ya mchakato wa kura za maoni za ubunge na udiwani, jijini Dar es Salaam na Lindi.
Kadhalika Takukuru inashikilia kiasi cha Sh. 1,677,000
kilichokutwa kwa makada hao kupitia mtego uliowekwa kwenye majimbo ya Wilaya ya
Kinondoni, jijini Dar es Salaam .
Makada hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
(UWT) kata ya Goba, Pili Mustafa, aliyekamatwa
saa 3 usiku akiwa na Sh. 1,330,000, Rehema Luwanja, anayegombea udiwani
kata ya Goba na Sh. 95,000, huku akiwa ameshagawa 110,000.
Wengine ni Katibu Itikadi wa CCM kata ya Kibamba, Babu
Kimanyo, aliyekamatwa saa 4:30 usiku akiwa na
Sh. 252,000 na tayari alishagawa sh. 330,000, Katibu CCM kata ya
Kibamba, Elias Nawera ambaye anagombea Ubunge Kawe, Siraju Mwasha anayegombea
udiwani Msigani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Denis Manumbu, alisema kuwa
mbali na watuhumiwa hao, wamepokea malalamiko 28 yanayohusu rushwa ambayo
wanayafanyia uchunguzi ili hatua zichukuliwe.
Alisema katika kipindi hiki cha kura za maoni za kuwapata
wagombea katika ngazi ya udiwani na ubunge katika vyama vya siasa majimbo manne
ya Wilaya ya Kinondoni, ofisi yake imepokea taarifa mbalimbali kutoka kwa
wananchi zinazohusu vitendo vya rushwa.
Manumbu alisema vitendo hivyo vinafanywa na watangaza nia na
wapambe wao na baada ya kupitia taarifa hizo ofisi ilizifanyia kazi na
kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao na kuwahoji.
Alisema ofisi yake ina mamlaka kisheria ya kumuita mtu
yeyote kutoa maelezo ili kusaidia uchunguzi wa tuhuma husika na mamlaka hayo
kwa mujibu wa kifungu cha 10(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya
mwaka 2007, atakayekiuka wito huo atakuwa amekwenda kinyume cha sheria.
Hata hivyo, alisema Takukuru inafanya kazi yake kwa mujibu
wa sheria na hawatasita kumchukulia hatua mgombea wa chama chochote na
upelelezi utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo vya dola.
LINDI WATIA NIA
UBUNGE CCM WANASWA
Huko Lindi, Takukuru, imewakamata na kuwahoji wagombea
wawili wa nafasi ya ubunge kupitia CCM kwa madai ya kutaka kuwahonga wajumbe,
wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Kamanda wa Taasisi hiyo, mkoani hapa, Stephen Chami,
amewaambia waandishi wa habari kuwa, wagombea hao wamekamatwa usiku katika
majimbo ya Lindi Mjini na Mchinga kati ya saa 5 usiku na 10-11 alfajiri ya
kuamkia jana.
Aliwataja wagombea na majimbo wanayogombea katika mabano
kuwa Mwekahazina wa Chama cha Walimu Taifa (CWT), Mohamedi Utali (Lindi mjini)
na mbunge viti maalumu aliyemaliza muda wake, Fatuma Mikidadi (Mchinga).
Alisema, Utali alikamatwa maeneo ya Mitwero, Manispaa ya
Lindi, kati ya saa 10-11 alfajiri, baada ya kupigiwa simu kutoka kwa baadhi ya
wananchi waliokuwa wamezingira gari, linalodaiwa kutumika katika harakati hizo.
“Baada ya wananchi kulishuku lile gari walilifuatilia na
kulizuia, na kupiga simu ofisini kwetu, ndipo nikaondoka mimi, vijana wangu na
askari polisi kuelekea Mitwero,” alisema.
Alisema muda ulipofika, waliwakuta wananchi wamelizingira
gari lenye namba za usajili T.563 BNA, na walipolipekuwa walifanikiwa kukuta
mfuko uliokuwa na fedha taslimu Sh. milioni 4.2.
“Zile fedha tulizozikuta zilikuwa ni noti za Sh. 2,000 na
Sh. 5,000,” alisema Chami.
Kamanda Chami alisema, Mikidadi alikamatwa Jimbo la Mchinga
saa 5 usiku na kufikishwa kwenye Ofisi ya Takukuru kwa mahojiano.
Alisema Mikidadi anadaiwa kutoa Sh. 780,000 kujaribu
kuwahonga maofisa wa Takukuru waliokuwa wanamhoji.
“Huyu mheshimiwa wakati akiendelea kuhojiwa aliwaomba awape
Sh. 780,000 alizokuwa nazo ili yaishe,” alisema Chami.
Aliongeza kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada
ya kukamilika kwa taratibu za ki-ofisi, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wao.
Watuhumiwa hao walipotafutwa na mwandishi wa habari hizi
kupitia simu zao za kiganjani ili kuzungumzia tuhuma hizo, simu zao zilizimwa.
Baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi wa CCM, walioshiriki
kufuatilia nyendo za wagombea wao na hatimaye kufanikisha kukamatwa kwao, huku
wakiomba majina yao
yasiandikwe gazetini, wamewaambia waandishi kuwa, kukamatwa kwao hakuna lengo
la kuwakomoa, bali ni kurejesha heshima ya chama kwa wananchi.
“Sisi ni miongoni mwa tulioshiriki kuanzia saa mbili usiku
hadi alfajiri, na wakati tukiwa kwenye doria hiyo, tulipigiwa simu na raia wema
kwamba kuna magari mawili, likiwemo Rav 4 rangi nyeupe ambaye ni mgombea ubunge
hapa jimbo la Lindi mjini,” alisema mmoja wao.
Hili ni tukio la pili kwa wagombea ubunge kupitia CCM mkoani
Lindi, kukamatwa na Takukuru. Juzi
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alihojiwa na taasisi hiyo.
